Huwel anusa ubingwa mbio za magari 2025

DEREVA kutoka Iringa, Ahmed Huwel amejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa taifa wa mbio za magari kwa mwaka huu kutokana na ushindi wake wa zile za Mkwawa zilizomalizika mkoani Morogoro mwishoni mwa juma.

Huwel, ambaye alimaliza wa tatu nyuma ya mabingwa wa Afrika; Karan Patel na Samman Vohra, alikuwa ndiye bingwa wa mashindano hayo kwa upande wa Tanzania.

Licha ya kuwa ni raundi ya tano ya Mbio za Magari Ubingwa wa Afrika, Mkwawa Rally of Tanzania, ilikuwa pia ni raundi ya nne ya mbio za magari ubingwa wa taifa (National Rally Championship) kwa mwaka 2025.

Huwel ambaye ameshacheza raundi mbili kati ya nne zilizofanyika mwaka huu, amewatoa kileleni Manveer Birdi wa Dar es Salaam, Gurpal Sandhu wa Arusha na Randeep Singh pia wa Dar.

Haya hivyo, hukumu ya azma yake kutwaa ubingwa wa taifa mwaka huu itafanyika mkoani Arusha na raundi ya tano na ya mwisho ya mbio hizo itachezwa Novemba 8, mwaka huu.

Birdi ndiye aliyeshinda raundi ya kwanza mkoani Iringa, wakati Randeep Singh alitwaa pointi zote 35 baada ya kushinda raundi ya pili jijini Dar es Salaam.

Huwel alichukua pointi zote 35 baada ya kushinda raundi ya tatu mkoani Morogoro kabla ya kushinda tena raundi ya nne hapo hapo Morogoro.

Upepo wa bahati pia umemsaidia Huwel kupaa juu ya wapinzani wake; Manveer, Singh na Sandhu, baada ya wote watatu kushindwa kumaliza raundi hii ya nne.

Guru Nanak Rally ndiyo jina la raundi ya hitimisho ya mbio za magari ubingwa wa taifa kwa mwaka huu na washabiki na wadau wana shauku ya kujua endapo gari ya kisasa ya daraja la mbio za magari za dunia (World Rally Championship), Toyota Yaris, itamfanya Huwel ashinde ubingwa wa taifa kwa mara ya kwanza na kuuondoa ufalme wa Mitsubishi kwa kuwashinda wapinzani wake ambao wote wanatumia gari aina ya Mitsubishi Evolution 1X.

Akiwa na Mitsubishi, Manveer Birdi ndiye bingwa mtetezi baada ya kuibuka mshindi wa jumla wa msimu uliopita.