Dar es Salaam. Watu saba sambamba na kampuni ya Jatu Public Limited, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 37 yakiwamo ya ubadhilifu wa fedha, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Jatu Saccos ya Sh3.149 bilioni.
Katika mashtaka hayo 37, 32 yanaikabili kampuni ya Jatu Public Limited ambayo ni kutakatisha fedha kwa kujipatia magari 25, pikipiki saba na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 500 kilichopo Kiteto mkoani Manyara.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Septemba 25, 2025 na kuunganishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Peter Gesaya, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili mahakamani hapo.
Washtakiwa hao ni Nicholaus Fuime, Esther Kiuya, Habiba Magero na Mariam Mrutu, Mariam Kusaja, Lucy Izengo na Kampuni ya Jatu Public Limited.
Kabla ya kusomewa kwa mashtaka yao, wakili wa Serikali, Roida Mwakamele alieleza Mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki kuwa wanaomba kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka chini ya kifungu 251(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Awali, kesi iliyokuwa inamkabili Gesaya ilisomeka kama kesi ya uhujumu uchumi 8 ya mwaka 2023 na sasa baada ya upande wa Jamhuri kufanya mabadiliko kwa kuongeza washtakiwa saba, kesi hiyo kwa sasa itasomeka kama kesi ya uhujumu uchumi namba 491356 ya mwaka 2025.
Kisha baada ya kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka, Hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa hao kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Vile vile, Hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa hao kuwa mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo watapelekwa rumande.
Hakimu Nyaki baada ya kutoa maelekezo hayo, aliruhusu upande wa mashtaka kuwasomea mashtaka hayo.
Hivyo, kwa sasa kesi hiyo mpya itakuwa na washtakiwa wanane akiwemo Gesaya.
Kati ya mashtaka 37 yanayowakabili washtakiwa hao, 33 ni ya kutakatisha fedha, moja kuongoza genge la uhalifu, ubadhilifu, matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia hasara Saccos ya Jatu.
Wakili Mwakamele alidai shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Januari 11, 2019 na Desemba 31, 2021 ndani ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walitengeneza genge la uhalifu kwa nia ya kufanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh3.149 bilioni, mali ya Jatu Saccos.
Shtaka la pili ni matumizi mabaya ya ofisi, linalowakabili Gesaya na Fuime, ambapo Februari 28, 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa watekelezaji wa majukumu yao kama Ofisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Jatu Saccos na Kampuni ya Jatu Public Limited, kwa pamoja walitumia nafasi zao vibaya kwa kusaini hati ya maridhiano ya Februari 28, 2019 kati ya Kampuni ya Jatu na Jatu Saccos na hivyo kukiuka kanuni za vyama vya ushirika na hivyo kupelekea Kampuni ya Jatu kupata faida ya Sh3.149 bilioni.
Shtaka la tatu ni ubadhilifu wa fedha na linawakabili Fuime, Kiuya, Magero, Mrutu, Kusaja na Izengo.
Washtakiwa kati ya Januari 11, 2019 nq Desemba 31, 2021 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa katika kutekeleza majukumu yao kama watia saini wa Jatu Saccos katika benki ya NMB kwa kukosa uaminifu na walitumia Sh763 milioni za Saccos kwa matumizi yao binafsi, fedha ambazo walikabidhiwa kutokana na nafasi zao.
Shtaka la nne ni kuisababishia Jatu Saccos hasara, linalowakabili washtakiwa wote.
Wakili Mwakamele alidai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2021 ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa makusudi, washtakiwa hao waliisababishia hasara Jatu Saccos hasara ya Sh3.149bilioni.
Vile vile, shtaka la tano ni utakatishaji linalowakabili washtakiwa wote, ambapo siku na eneo hilo, walijihusisha na muamala wa moja kwa moja na kupata kiasi Sh3.149, bil wakati mkijua kuwa fedha hizo ni mazalia ya uhalifu ambayo ni ubadhilifu.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa shtaka la sita hadi la 36 ni utakatishaji fedha na linamkabili mshtakiwa wa nane ambaye ni kampuni ya Jatu Public Limited.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kuanzia Julai Mosi, 2017 hadi Februari 25, 2025 katika Jiji la Dar es Salaam, kampuni hiyo ilijipatia magari 24 na pikipiki saba aina ya Fekon, wakati wakijua fedha zilizotumika kununu vyombo hivyo ni mazalia ya kosa tangulizi la matumizi mabaya ya fedha na ubadhilifu.
Hata hivyo, kati ya magari hayo 25; yapo matrekta matano, mashine moja ya kuvunia mazao, malori mawili , Toyota Land Cruiser Prado moja, Toyota IST tatu, Nissan Xtrail mbili, Mistubishi Center, Toyota Alphad mbili, Noah, Funcargo, Rav4, Mark ll na New Holland.
Shtaka la 37 pia ni utakatishaji na linaikabili kampuni ya Jatu Public Limited, ambapo katika kipindi hicho eneo la matui wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, kampuni hiyo ilijipatia shamba moja namba 288 lenye ukubwa wa ekari 500, wakati wakijua kuwa fedha za ununuzi wa eneo hilo, zilitokana na mazalia ya kosa tangulizi la matumizi mabaya ya fedha na ubadhilifu wa fedha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wapo katika hatua za kuandaa taarifa ili waziwasilishe Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 8, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.