:::::::::
Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Tanzania, Getrude Mpangile, amesema kampuni hiyo imetoa Elimu ya usalama barabarani katika Shule ya Msingi Mnadani Septemba 24,2025 ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika katika Mkoa wa Dodoma.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwafundisha watoto sheria na kanuni za usalama barabarani ili waweze kutumia barabara kwa usahihi wanapokwenda na kurejea shuleni.
Aidha, Amebainisha kuwa kwa mwaka huu jumla ya shule saba zinashiriki kwenye programu hiyo, ikiwemo shule moja ya wanafunzi wenye ulemavu, ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Aidha, Getrude Mpangile amesema watoto hufundishwa elimu ya usalama barabarani kupitia sanaa mbalimbali ikiwemo uchoraji, uimbaji na maigizo kwa kushirikiana na shirika la Nafasi Art Space ,
Pia, amesema kuwa Shule ya Msingi Makuburi ilifanikiwa kushinda katika mashindano ya usalama barabarani, hatua ambayo imezaa matokeo chanya kwa usalama wa wanafunzi. kutokana na ushindi huo, shule hiyo ilijengewa ukuta ili kuongeza usalama wa watoto wanapovuka barabara na kutembea ndani ya eneo la shule.
Aidha, amebainisha kuwa mashindano ya elimu hiyo yanayofanyika katika ngazi ya kitaifa, Afrika na hatimaye ngazi ya kimataifa Jijini Paris, Ufaransa.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mnadani, Gesi Janken, amesema elimu hiyo imesaidia wanafunzi kutumia barabara kwa usalama kwani shule ipo karibu na barabara kuu na awali kulikuwa na changamoto za ajali za mara kwa mara.
Kwa upande wake Felix Mchira , Mratibu wa Nafasi Art Space, amesema wamechagua kutumia sanaa kufundisha usalama barabarani kwa kuwa ni rahisi kueleweka kwa watoto kwani alama nyingi za barabarani ni michoro na picha.
Aidha, Amesema kuwa mradi huu umefanyika Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na sasa Dodoma, na umekuwa na mwitikio mkubwa, pia amebainisha kuwa Shule zinazoshinda hupata zawadi.
Aidha, wanafunzi wa shule hiyo wameeleza namna walivyonufaika na elimu hiyo. Jasmin Yasin, mwanafunzi wa darasa la sita, amesema ”wamejifunza kuhusu alama za barabarani, ikiwemo kutambua zebra crossing na kupita upande wa kulia wanapokuwa barabarani”
Asha Abdallah, mwanafunzi mwingine, amesema ”elimu hiyo imewasaidia kuvuka barabara kwa usalama kwa kuangalia upande wa kulia, kushoto na tena kulia kabla ya kuvuka”.
Kwa upande wake mwanafunzi Bon Joseph ametoa shukrani kwa elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani kwa kuwaelimisha wanafunzi wengine.
Aidha, Wanafunzi hao kwa pamoja wameahidi kuzingatia alama za usalama barabarani na kutoa elimu kwa wenzao ili kupunguza ajali.