Jaji Mkuu Masaju: Upelelezi dhaifu unawapa nafasi wahalifu kuachiwa

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amesema udhaifu katika mifumo ya upelelezi umekuwa chanzo kikuu cha wahalifu wengi kuachiwa huru mahakamani.

Akitolea mfano wa hali ilivyo sasa, amesema baadhi ya watuhumiwa wanaendelea kurudia makosa mara kwa mara kwa sababu wameshajua mianya na upungufu uliopo kwenye mchakato wa upelelezi.

Akizungumza jana, Septemba 24, 2025, wakati wa kufungua mkutano maalumu wenye ajenda kuu ya “Ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji  haki” uliofanyika katika ukumbi wa mikutano ya Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Masaju amesema changamoto hiyo ni ya muda mrefu na sasa ni lazima ichukuliwe hatua mahsusi.

“Faida ya kwanza ya kuimarisha upelelezi ni kwamba tutajua mapema kama shauri lina msingi wa kisheria au la. Tukipeleleza kwa umakini, tutapunguza idadi ya kesi zisizo na ushahidi wa kutosha na hivyo kuzuia wahalifu wanaoachiliwa kwa upungufu wa upelelezi. Kwa kufanya hivyo, tutapunguza vitendo vya uhalifu vinavyorudiwa mitaani,” amesema.

Jaji Masaju amefafanua kuwa mara nyingi mahakama zimekuwa zikishughulikia mashauri yasiyo na vielelezo vya kutosha, hali inayosababisha kubambikiziwa kesi kwa watu wasio na hatia na magereza kujaa zaidi ya uwezo wake.

“Kukamilika kwa mpango huu, waendesha mashtaka na mahakama watalazimika kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kupeleka kesi mahakamani. Hii itasaidia pia kupunguza ubambikizaji wa kesi na msongamano usio wa lazima magerezani,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, Jaji Masaju ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuacha kuwawakilisha au kuwatetea watu wanaoshtakiwa kwa kesi za madai.

“Hizi ni kesi za madai. Wengine wanashtakiwa, mnaenda mnawatetea. Waacheni wapambane na hali zao wenyewe. Haiwezekani mtu akibambikiza kesi atetewe kwa kisingizio cha kutekeleza majukumu ya ofisi. Hii ni matumizi mabaya ya madaraka. Kama kuna kesi kama hizo, wacha DPP azisimamie kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Ameongeza kuwa hatua hiyo itaimarisha nidhamu ya utumishi wa umma, kuongeza uadilifu na kuharakisha upelelezi kwa makini bila ucheleweshaji.

Rushwa inavyodhoofisha haki

Jaji Masaju hakusita kugusia changamoto ya rushwa, akibainisha kuwa bado ipo ndani ya taasisi muhimu za utoaji haki.

“Hatuwezi kujificha. Ni kweli rushwa ipo. Ipo polisi, ipo mahakamani na ipo kwenye taasisi nyingine za Serikali. Ripoti nyingi zimebainisha hilo waziwazi,  ndiyo maana tumesisitiza kuimarisha mifumo ili kupunguza mianya ya vitendo hivi,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa hatima ya muhimili wa Mahakama kufikia hadhi iliyokusudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan itategemea zaidi nidhamu, uwajibikaji na kupambana na rushwa ndani ya taasisi.

Jaji Masaju amewaomba pia wanachama wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kuchukua wajibu wao kwa uzito katika mashauri mbalimbali wanayoshiriki, iwe ni ya jinai, madai au kikatiba.

“Wanasheria wa TLS, jukumu lenu ni kuhakikisha mnasimama ipasavyo kuwatetea wateja wenu. Hapa mahakamani tutaendelea kuimarisha usimamizi wa kinidhamu kuhusu nyinyi pia. Kila mmoja ni lazima atimize wajibu wake kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Akizungumzia umuhimu wa kasi ya utoaji haki, Jaji Masaju amesema ni kinyume cha Katiba kumpeleka mtu mahakamani bila ushahidi wa kutosha.

“Ibara ndogo ya 6 ya 13(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila anayeshtakiwa atachukuliwa kuwa hana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo na mahakama.

“Lakini hali ilivyo sasa, mara nyingi watu wanapelekwa mahakamani wakiwa hawajui ni ushahidi upi upo dhidi yao, na hata mahakama yenyewe inashindwa kufanya uamuzi sahihi kwa kukosa vielelezo vya kutosha. Hili ni jambo lisilokubalika,” amesema kwa msisitizo.

Pia amesisitiza kuwa mshikamano wa pamoja kati ya vyombo vyote vya kisheria, Serikali na taasisi za kiraia ni sharti la kikatiba na kisheria na takwa la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tusiposhirikiana, hatuwezi kufanikisha malengo ya haki kwa wote. Lazima kila upande—Mahakama, Polisi, waendesha mashtaka, wanasheria na wananchi uchukue wajibu wake. Hapo ndipo haki ya kweli itapatikana kwa wakati,” amesema.