Aliyekutwa akisafirisha kokeni jela maisha

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ,imemuhukumu kifungo cha maisha jela, Hemed Mrisho, maarufu Horohoro baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya kokeni gramu 326.46.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 23, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi ya mwaka 2024 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Katika kesi hiyo ilielezwa mahakamani hapo kuwa Oktoba 31, 2023 katika eneo la Boko Magengeni, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, Hemed alikutwa akisafirisha dawa hizo za kulevya.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 34390/2024, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 14 na vielelezo 23 huku mshtakiwa huyo akiwa shahidi pekee wa utetezi.

Shahidi wa nne, Inspekta Paschal Daudi, alielezwa siku ya tukio wakati DCEA (Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya) wanaendelea na doria yao ya kawaida eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, walipokea taarifa kuna biashara ya dawa za kulevya inafanyika katika eneo la Tegeta na mshukiwa alikuwa akisafiri.

Alidai walijulishwa Hemed aliyekuwa akiendesha gari nyeupe aina ya BMW X 5, ndiye alikuwa na dawa hizo za kulevya ambapo waliamua kuweka mtego na kufuatilia gari hilo ambapo walishirikiana na trafiki katika eneo hilo.

Shahidi wa 10, Sajenti Joseph alidai mahakamani hapo walizuia gari hilo na kumuweka mshtakiwa chini ya ulinzi kisha wakamjulisha kuwa anatuhumiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Alidai walitafuta shahidi wa kujitegemea ambapo walipofanya upekuzi walimkuta na bastola, risasi saba, vitambulisho kadhaa, kadi za benki, fedha Sh4.1 milioni,mfuko wa nailoni uliokuwa na unga mweupe ambao ulishukiwa kuwa ni dawa za kulevya pamoja na nyaraka zingine.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa sampuli za unga huo zilipelekwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), na majibu yalionyesha ni dawa za kulevya aina ya kokeni yenye uzito wa gramu 326.46.

Akijitetea mahakamani hapo, Hemed alidai kukamatwa Oktoba 27,2023 saa 11 jioni akiwa soko la Tandale akiendelea na biashara zake na kupelekwa ofisi za DCEA zilizopo Kivukoni, ambapo alidai kukamatwa akiwa na bastola, pochi, Sh150,000.

Alidai kuwa alishinikizwa huku akipigwa na kushinikizwa atoe taarifa ilipo shehena na kuwa alimsikia mtu aitwaye Salmin ambaye wanatoka kijiji kimoja cha Sonde (Lushoto) na kuwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi kati ya wazazi wao, hivyo  kulikuwa na uadui baina yao uliomsababishia amtengenezee kesi hiyo.

Mshtakiwa huyo alikana kusaini hati ya ukamataji, kumiliki gari lolote na kuwa hajui hata kuendesha gari na kuiomba mahakama imuachie huru kwa madai hahusiki na biashara ya dawa za kulevya.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Kisanya amesema Mahakama katika kufikia uamuzi wake itazingatia ikiwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Amesema suala hilo limejikita katika misingi ya sheria, hususan vifungu vya 3(2)(a) na 121(1) vya Sheria ya Ushahidi na imesisitizwa mara kadhaa kwamba katika kesi za jinai mzigo wa uthibitisho uko kwa upande wa mashtaka na kwamba kiwango kinachohitajika.

Jaji Kisanya amesema kwa kuzingatia yaliyotangulia ni muhimu kutambua kuwa chini ya vifungu vya 15(1)(a) na (3)(i) vya Sheria ya DCEA, kosa la kusafirisha dawa za kulevya hubainika pale mtu anaposafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa zaidi ya gramu 200.

Jaji amesema katika utetezi wa mshtakiwa amedai alikamatwa Oktoba 27, 2023 wakati kosa linadaiwa kutokea Oktoba 30,2023 na kuwa awali wakati wa maelezo ya awali, mshtakiwa hakuileza mahakama kuwa atatoa utetezi wa kutokuwepo eneo la tukio tarehe husika ya tukio hilo.

Baada ya kupitia hoja hizo amesema miongoni mwa masuala Mahakama inayozingatia ni iwapo dawa hizo za kulevya zilikamatwa kwa Hemed, kama upekuzi na ukamataji ulifanywa kihalali, kama mlolongo wa ulinzi ulitunzwa ipasavyo.

Jaji Kisanya amesema baada ya kuzingatia ushahidi wa pande zote mahakama inamkuta Hemed na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya kokeni iliyokuwa na uzito wa gramu 326.46.

“Kwa mantiki hiyo namkuta Hemed ana hatia chini ya kifungu cha 15(1)(a) na (3)(i) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, na masharti ya kifungu cha 60(2) cha EOCCA ambayo inaeleza hukumu ya lazima ya kifungo cha maisha,” amesema.

Jaji huyo alihitimisha kwa kutoa amri tano kuhusu vielelezo ikiwemo kuharibiwa kwa dawa hizo za kulevya kwa mujibu wa sheria, simu, kadi za benki, kadi  ya usajili wa gari na makubaliano ya mauzo ya gari na mkoba wenye nguo utarudishwa kwa mshtakiwa ambaye zilikamatwa kutoka kwake.

Nyingine ni silaha na risasi zake kukabidhiwa kwa msajili wa silaha ili ishughulikiwe kwa mujibu wa sheria, ambayo inaweza kujumuisha kuzirejesha kwa mtuhumiwa, ikibidi.

Kuhusu fedha Sh4.1 milioni, gari na ufunguo wake upande wa Jamhuri umeelekezwa kuchukua hatua stahiki chini ya kifungu cha 53 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.