MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Jonathan Sowah, leo ndiye aliyepewa jukumu la kuongoza mshambulizi ya timu hiyo katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Fountain Gate inayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Hii ni mechi ya kwanza ya kimashindano kwa Sowah kubebeshwa jukumu hilo, awali alikosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa msimu uliopita kwenye fainali ya Kombe la FA wakati huo akiichezea Singida Black Stars.
Mbali na Sowah ambaye msimu uliopita alipachika mabao 13 katika Ligi Kuu Bara akiwa na Singida Black Stars, mabadiliko mengine ambayo yameonekana kwenye kikosi cha Simba ukilinganisha na kile kilichoanza katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United huko Botswana ni pamoja na Mzamiru Yassin.
Awali Mzamiru hakuwa na nafasi kwenye kikosi cha Fadlu Davids ambaye ameachana na wekundu hao wa Mwimbazi siku chache zilizopita na kujiunga na Raja Casablanca.
Kikosi kamili cha Simba kimeanza hivi; Moussa Camara, Shomari Kapombe, Naby Camara, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, Yussuph Kagoma, Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Sowah, Jean Charles Ahoua na Ellie Mpanzu.
Kwa upande wa Fountain Gate, ina kikosi chenye jumla ya wachezaji 13 ambao kati yao 11 wameanza huku wawili wakikaa benchi.

Fountain Gate walioanza ni Fadhil Kisunga, Daniel Jolam, Elie Makono, Abdallah Kulandana, Lamela Maneno, Sadick Ramadhani, Jackson Katanga, Shaaban Pandu, Mudrick Abdi, Shomari Mussa na Hassan Ally. Benchi kuna Anack Mtambi na Machupa Juma.