YANGA imeanza kwa kishindo Ligi Kuu kwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji na kuwafanya mashabiki kuifurahia ushindi huo mnono licha ya kutofurahishwa na jinsi timu ilivyocheza, lakini Kocha Romain Folz amewashusha presha, huku akijifungia na mastaa na kuwawashia moto.
Watetezi hao wa Ligi Kuu na Kombe la FA, ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mabao ya Lassane Kouma katika kipindi cha kwanza na mengine mawili ya Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya katika kipindi cha pili, lakini namna kikosi hicho kilichocheza dakika 50 za kwanza kiliwanyima raha mashabiki na baadhi ya mabosi wa timu hiyo.
Baada ya mchezo huo kumalizika kocha Folz, alikuwa mkali kwa wachezaji wa timu hiyo hasa wale waliocheza dakika 45 za kwanza, akiwapa ukweli kwamba kila mmoja anatakiwa kujitathimini kama anatosha ndani ya kikosi hicho.
Inaelezwa mapema Folz alikuwa mkali kwa wachezaji huku akishusha mikwara mzito wa kumtupa mchezaji yoyote benchi, endapo kila alipewa nafasi atashindwa kuonyesha kiwango kizuri.
Pengine mkwara huo ndio uliokwenda kubadilisha mambo kwa kutengeneza mabao mawili yaliyokuja kuwashusha presha mashabiki wa timu hiyo.
Akizungumzia hilo, kocha huyo raia wa Ufaransa alisema anaelewa ambapo mashabiki wakiona timu yao haikucheza vizuri kipindi cha kwanza na kwamba hilo analibeba yeye kwanza, kisha kulishusha kwa wachezaji wake.
Folz alisema alilazimika kufanya mabadiliko makubwa kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wengine, lengo lilikuwa ni kukabiliana na ratiba ngumu ya mechi za karibu, kwani tangu itoke kucheza mechi ya Wiki ya Mwananchi Septemba 12, Yanga imeshacheza mechi tatu mfululizo ndani ya muda mfupi, ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika na hiyo ya Ligi Kuu.
Kesho Jumamosi itashuka tena uwanjani kubaliana na Wiliete Benguela ya Angola katika meci ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kusafiri ili kuifuata Mbeya City itakayovaana nao Septemba 30, jijini Mbeya.
“Bila shaka nakubaliana na kila mmoja hatukucheza vizuri dakika 45 za kwanza, tulijiweka kwenye presha badala ya kuwapa presha hizo wapinzani, sio mashabiki hata mimi sikuvutiwa, nawaelewa,” alisema Folz na kuongeza;
“Kama kocha nabeba hilo kwanza baada ya hapo nakwenda kuongea na timu nzima, unapokuwa mchezaji wa klabu kama hii unatakiwa kuwa tayari kufanya kikubwa kwa uzito wa jezi ya timu hii.
Hatukuwa na chaguo lingine zaidi ya kubadilisha kikosi ili kulinda viwango vya wachezaji, ratiba yetu ngumu sana, kuna wakati tunatakiwa kufanya rotesheni kubwa ili kulinda afya pia za wachezaji.”
Katika mechi hiyo ya juzi Yanga ilifanya mabadiliko ya wachezaji nane tofauti na kikosi kilichocheza ugenini dhidi ya Wiliete kilichoshinda 3-0 na watatu pekee walianza akiwamo kipa Djigui Diara na mabeki Bakari Mwamnyeto na Israel Mwenda, huku wengine wakiingia kipindi cha pili akiwamo Aziz Andabwile, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua walioipa timu uhai.