Mashahidi 13 kutoa ushahidi, kesi ya kusafirisha kilo 51 za heroini

Dar es Salaam. Mashahidi 13 na vielelezo 16 vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 51.47 inayomkabili mkazi wa Kawe, Ernest Semayoga (48) na wenzake watatu.

Mbali na Semayoga maarufu Mukri na washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Salum Jongo (45) mkazi wa Mbezi Beach, Amin Kesibo (25) ambaye ni mkulima na mkazi wa Mbezi Beach pamoja na Tatu Nassoro (45) mjasiriamali na mkazi wa

Veterinary Wilaya ya Temeke.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja la kusafirisha kilo 51.47 za heroini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao,  Mahakama Kuu, pindi kesi hiyo itakapopangiwa tarehe ya kusikilizwa, baada ya  leo,  Alhamisi Septemba 25, 2025 washtakiwa hao kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Hatua hiyo imekuja baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Hii ni mara ya pili kwa washtakiwa hao kusomewa Commital Proceedings, kwani Aprili 8, 2024 washtakiwa hao walisomewa maelezo hayo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 78 ya mwaka 2020 katika Mahakama ya Kisutu na kisha  kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Agosti 2025 washtakiwa hao walifutiwa kesi yao iliyokuwa na mashtaka matatu Mahakama Kuu na kurudishwa Mahakama ya Kisutu, ambapo walisomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka moja.

Hata hivyo, leo Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas, ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantu Mwankuga, wakati akiwasomea  washtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Wakili Protas alidai vielelezo 16 ni vya nyaraka na vielelezo 11 ni nyaraka halisi ikiwemo hati ya ukamataji mali,  ripoti kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kiasi cha dawa kilichokamatwa kwa washtakiwa hao, maelezo ya onyo ya washtakiwa wote na  fomu ya uwasilishaji wa sampuli kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Protas baada ya kueleza hayo aliwasomea upya shtaka lao na kisha maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwankuga aliwaambia washtakiwa hao kuwa kesi yao ameihamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji na wakati wakisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, washtakiwa hao watakuwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.