Arusha. Wanafunzi watatu kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), wamebuni roboti lenye uwezo wa kukagua chupa za vinywaji katika mchakato wa uzalishaji viwandani.
Mashine hiyo iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa Profesa Anaeli Sam, Dk Judith Leo na Jared Nganyi, inafanya kazi kwa mfumo wa kunyanyua na kushusha, ikiwa na mkono wa roboti pamoja na kamera yenye akili bandia (AI), inayoweza kutambua usahihi wa umbo na rangi kabla ya kushughulikia kitu.
Sehemu ya mwisho ya roboti hiyo inaweza kubadilishwa na vifaa mbadala kama vile kifaa cha kunyonya na kubeba, jambo linaloliwezesha kufanya kazi nyingi kulingana na mahitaji ya kiwanda.
Akizungumza kuhusu ubunifu huo leo Alhamisi Septemba 25, 2025, Dk Leo amesema waliamua kutengeneza roboti hiyo kutokana na changamoto zilizopo viwandani na binadamu wanaofanya kazi za ukaguzi mara nyingi hushindwa kufanikisha majukumu yao kwa ufanisi, na hujikuta katika hatari ya kujeruhiwa na mashine.
“Baada ya kuibuni mwaka jana, tulifanya majaribio katika kiwanda cha Bia cha Tanzania Breweries Ltd (TBL) jijini Arusha na matokeo yalionyesha ufanisi mkubwa,” amesema Dk Leo na kuongeza kuwa, “kwa sasa tumeanza mazungumzo na baadhi ya viwanda ili kutengeneza mashine kubwa zaidi na kuwauzia kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wao.”
Kwa niaba ya wabunifu, Daniel Msilange amesema mfumo huo umebuniwa kwa lengo la kuongeza usahihi, ufanisi na usalama wa bidhaa kwa kukagua chupa zinazotoka kwenye laini ya uzalishaji. Roboti hilo hufanya kazi ya kukagua usafi, uimara, uhalisia na viwango vya kioevu.
“Endapo roboti litabaini chupa yenye kasoro, iliyochafuliwa au kujazwa vibaya, huiondoa mara moja kutoka kwenye laini ya uzalishaji ili kuhakikisha bidhaa bora pekee ndizo zinamfikia mlaji,” amesema Msilange.
Ubunifu huo uliwasilishwa wakati wa ziara ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa, Fred Msemwa, alipotembelea chuo hicho kujionea bunifu mbalimbali na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Msemwa pia alishuhudia bunifu zingine ikiwemo mashine ya kuchakata ngozi, teknolojia ya kusafisha maji, nishati jadidifu na bidhaa za lishe ya mifugo.
“Tumetiwa moyo na hatua hizi. Zinaonyesha taasisi hii iko tayari kuchukua nafasi kubwa katika kusukuma uchumi wa kidijitali unaotegemea sayansi na ubunifu,” alisema.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Maulilio Kipanyula amesema kinazalisha bunifu nyingi ambazo zingekuwa na mwendelezo bora zaidi kama kungekuwa na Hifadhi ya Kitaifa ya Teknolojia.
Ametoa wito kwa Serikali kuanzisha hifadhi hiyo ili kuharakisha ubia wa bunifu za ndani na kuzigeuza bidhaa zinazoweza kuingia sokoni, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na ajira.
Profesa Kipanyula ameongeza kuwa NM-AIST inalenga kujenga ikolojia ya ubunifu jijini Arusha itakayovutia vipaji vya ndani na kimataifa, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya nchi kuelekea uchumi wa maarifa na kidijitali.