Samia: CCM ndiyo italinda na kuinua utu wa Mtanzania

Lindi. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan amesema hakuna chama kitakachoweza kulinda na kuinua utu wa Mtanzania kama chama chake, hivyo ifikapo Oktoba 29 wananchi hawapaswi kufanya makosa.

Samia ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimbo la Mchinga ambapo pamoja na kuomba ridhaa ya urais  alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Salma Kikwete.

“Tupeni ridhaa yenu tuendeshe nchi hii kwa miaka mitano ijayo, tufanye kazi ili tuinue utu wa Mtanzania. Tunapozungumzia utu ni kuwapatia watu elimu, huduma za afya, maji, huduma za umeme, kilimo chenye tija huo huduma nyingine muhimu, hii ndiyo kulinda na kukuza utu wa mtu.

“Ukisoma ilani yetu tunakwenda kufanya kazi ili kulinda utu wa Mtanzania, nimesikia na wengine wanapita huko na kusema yaliyopo kwenye ilani yetu unasikia mtu anasema ataleta maji mara elimu bure alikuwa wapi siku zote asilete kama sio maneno ya uongo,” amesema mgombea huyo.

Amesema akipata ridhaa ya kuwa Rais kwa miaka mitano ijayo, Serikali yake itaendeleza miradi iliyoenza na kutekeleza mipya ambayo imehainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya 2025/2030.

Kwenye upande wa sekta ya maji amesema mbali na mradi unaotekelezwa vitaongezwa visima lengo likiwa kuongeza upatikanaji wa maji na kuhakikisha kila Mwanamchinga  anafaidika na maji safi na salama.

Kwenye eneo la kilimo amesema ataendeleza mpango wa ruzuku za pembejeo ili kustawisha kilimo cha korosho kuwezesha zao hilo kupatikana kwa wingi.

“Hizi ruzuku tunazotoa lengo ni kuwapa nafuu wakulima wahudumie mashamba yao vizuri ili wapate mazao ya kutosha. Tutaendelea pia kutafuta masoko yenye bei kubwa, mfumo wa stakabadhi ghalani umefanya kazi nzuri, ilikuwa ngumu kukubalika lakini sasa unafanya vizuri.

“Tutakwenda kuongeza huduma za ugani kwa kuwawezesha maofisa ugani ili waweze kufuatilia kilimo chetu. Kingine ni kuimarisha na skimu za umwagiliaji kutoa fursa kwa wakulima kulima mara mbili kwa mwaka,” amesema.

Pia mgombea huyo ameahidi jimbo hilo kupata kiwanda cha kuongeza thamani ya mwani endapo itaonekana zao hilo linazalishwa kwa wingi katika eneo hilo la Mchinga.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Salma Kikwete amesema wananchi wa Mchinga wana matumaini makubwa na miaka mitano ijayo ya uongozi wa Samia.

Amesema jimbo hilo limepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, miundombinu na umeme.

“Tumeshuhudia utekelezaji kwa vitendo wa dhamira ya kumtua mwanamke ndoo kichwani, tumepata mradi wa maji uliogharimu Sh10 bilioni, kabla ya hapo wana Mchinga walikuwa wakipata maji ya visima.

“Bado kuna vijiji vina changamoto ya maji lakini kwa kura tutakazokupatia ni imani yetu miradi mingine ya maji itakuja na changamoto hii itakuwa historia,” amesema Salma.

Kwa upande huduma wa afya amesema katika kipindi cha miaka mitano zimejengwa zahanati na kituo cha afya ambacho kimesaidia kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Kwenye nishati amesema vijiji vyote 47 vya Mchinga vimeunganishwa umeme na kufikia sasa vimesalia vitongoji 32 pekee ambavyo havijaunganishwa na huduma hiyo.

Salma amesema endapo wananchi wa Mchinga watampa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo ataendeleza jitihada zake za kusaidia michezo akiwa na lengo la kuhakikisha timu kutoka jimbo hilo inashiriki kwenye ligi kuu.

“Tumeshirikiana vyema na wananchi wa Mchinga katika kipindi cha miaka mitano, nimewaitikia kila mliponiita, nimesikiliza naomba mnichague ili niwatumikie kwa kipindi kingine cha miaka mitano,” amesema Salma.

Jimbo la Mchinga linalojulikana kwa shughuli za kilimo cha korosho, mihogo na ufuta, linaelezwa kuwa nyuma kimaendeleo licha ya uwepo wa ardhi yenye rutuba na rasilimali nyingi za bahari.

Wananchi wanasema kwa miaka mingi wamekuwa wakiahidiwa miradi mbalimbali lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu, hali inayosababisha kupoteza imani na maneno ya wanasiasa.

Baadhi ya wakazi wa jimbo hilo waliozungumza na Mwananchi wameeleza  wanataka mbunge atakayeweka kipaumbele kwenye kushughulikia changamoto hizo na sio kutoa ahadi zisizotekelezeka.

“Kiongozi tunayemtaka si wa maneno, tunataka mtu mwenye uwezo wa kushawishi Serikali kuleta barabara bora, maji na elimu bora. Tumekaa muda mrefu tukisubiri maendeleo,” amesema mkazi wa kijiji Mingumbi, Hassan Mzee.

Kwa upande wake Salum Chomolo amesema wana Mchinga wanataka mbunge atakayekuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao mara kwa mara.

“Tunataka mtu atakayekaa na sisi vijijini, atakayetuita kwenye mikutano na kusikiliza shida zetu. Siyo kuja wakati wa kampeni tu na kuondoka,” amesema Chomolo ambaye ni mkulima katika jiji cha Rutamba.

Kuhusu tatizo la ajira vijana wameeleza kuwa limechangia baadhi yao kuingia kwenye vitendo vya kihalifu au kujihusisha na uvuvi usio endelevu.

“Tunahitaji kiongozi atakayetuwezesha kupata mafunzo ya ufundi stadi, kutupatia mikopo midogo na kutusaidia kuanzisha miradi ya kujiajiri. Vijana wengi tumebaki bila ajira na hii inaleta hasara kubwa kwa jamii,” amesema  Sharifu Jongo.