Mwanza. Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Loveness Kisile (30), mkazi wa Mtaa wa Temeke, jijini Mwanza akituhumiwa kutoa taarifa za uongo kwa askari, ndugu, jamaa na marafiki kuwa ametekwa.
Anadaiwa kutoa taarifa kwa mume na ndugu zake kwamba ametekwa na watu watatu waliotaka Sh10 milioni ili wasimdhuru na kuondoa ujauzito aliokuwa nao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Septemba 24, 2025 saa 5:30 usiku, baada kumpigia simu mume wake, Hosea Lusingwa akidai watu hao walimkamata kwa nguvu, kumfunika uso na kumpeleka kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Septemba 25, 2025 Kamanda Mutafungwa amesema taarifa hizo zilizua taharuki kwa mume na ndugu na kulihangaisha Jeshi la Polisi usiku kucha, kwani awali Loveness alimweleza mume wake kwamba ni mjamzito wa pacha watatu.
Amesema mume alitoa taarifa Kituo cha Polisi Nyakato akidai watekaji wanahitaji Sh10 milioni na kama asingefanya hivyo wangemchoma mke wake sindano ya kutoa mimba.
”Baada ya muda mfupi alimjulisha mume wake kuwa mimba imetolewa na watoto wake pacha watatu wamefariki dunia, akisisitiza atume kiasi hicho cha fedha ili aachiwe huru,” amesema.
Kamanda Mutafungwa amesema upelelezi wa tukio hilo ulianza na ilipofika Septemba 25, 2025 saa 10:00 usiku, askari walimpata Loveness akiwa salama katika Mtaa wa Mecco, Kata ya Buzuruga, wilayani Ilemela, huku nguo akiwa amezichana.
Amesema baada ya kukamatwa na kuhojiwa, mtuhumiwa alikiri kutoa taarifa za uongo kwamba ametekwa na mimba imetolewa.
”Mtuhumiwa alipelekwa hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu na kuthibitika hajawahi kupata ujauzito. Kutokana na maelezo hayo mtuhumiwa alihojiwa tena kwa kina juu ya taarifa za kutekwa kama alivyowapatia wakwe na mume wake,” amesema.
Amesema baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alieleza kwamba alifanya hivyo ili kumdanganya mume wake na wakwe zake ili waendelee kumuamini na watoe mahari nyumbani kwao.
”Fedha alizokuwa anadai zitumwe alikuwa anazihitaji kwa manufaa yake,” amesema.
Kamanda Mutafungwa ametoa onyo kali kwa wananchi kuhusu kutoa taarifa za uongo za matukio ya uhalifu, hususani yanayohusisha vitendo vya kihalifu vya kutekwa, kudhulumiwa au kufanyiwa ukatili kwa lengo la kuficha ukweli, kujipatia huduma na msaada wa kifedha kutoka kwa watu mbalimbali.
”Matukio haya yanaleta hofu na taharuki zisizo za msingi kwa jamii. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo,” amesema.