:::::::
Kilombero
Mkuu wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Mh. Dunstan Kyobya amesema wilaya anayoiongoza ina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vimekuwa vikichangia makusanyo ya Kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo leo tarehe 25.09.2025 wilayani Kilombero alipotembelewa na maofisa wa TRA wanaoendesha zoezi la kutoa elimu ya Kodi mlango kwa mlango wilayani humo ambao wanaendelea na zoezi hilo katika Halmashauri za Ifakara na Mlimba.
Mhe. Kyobya amesema wilaya ya Kilombero inavyo vyanzo vingi vya mapato ambavyo ndiyo vyanzo vya kodi ikiwemo Sekta ya Utalii, Viwanda hususan kiwanda cha sukari, biashara pamoja na kilimo jambo ambalo linawatofautisha Kilombero na wilaya nyingine.
“Sisi hapa arthi yetu inakubali mazao ya kila aina ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangamsha uchumi wetu, ikiwemo Miwa, Kahawa, Kokoa, Ufuta na Viungo vya kila aina jambo ambalo ni la kujivunia maana uchumi wa wananchi unaendelea kuimarika huku wakichangia makusanyo ya kodi” amesema Mhe. Kyobya.
Amesema akiwa ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya ushauri ya kodi wilayani humo amekuwa akishirikiana kwa karibu na TRA kuhakikisha malengo ya makusanyo ya kodi wilayani humo.
Kwa upande wake Meneja wa TRA wilaya ya Kilombero Bw. Innocent Minja amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kushirikiana na TRA katika kuhamasisha ulipaji wa Kodi kwa hiari jambo ambalo limeongeza makusanyo na wigo wa kodi.
“Tunashirikiana kwa karibu sana na Mkuu wetu wa wilaya katika kuhamasisha masuala ya kodi na kuongeza wigo wa kodi kupitia vyanzo vipya” amesema Bw. Minja.
Kuhusiana na zoezi la kutoa elimu ya kodi mlango kwa mlango wilayani Kilombero Kiongozi wa zoezi la elimu ya mlango kwa mlango Afisa Habari Mkuu wa TRA Bw. Macdonald Mwakasendile amesema zoezi hilo linalenga kuwasikiliza Walipakodi, kutatua changamoto zao na kuwashukuru kwa kuendelea kulipa Kodi huku wakiwakumbusha kulipa Kodi ya awamu ya tatu inayoishia Septemba 30.
= = = = = = =