Mbeya. Mgombea ubunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson ameahidi kuchimba visima vikubwa katika kata ya Itezi ili kumaliza adha ya maji kwa wananchi wake ikiwa ni miongoni mwa vipaumbele vyake katika jimbo hilo.
Vipaumbele vingine alivyojiwekea Dk Tulia ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara na kusimamia utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ili wajikwamue kiuchumi.
Amesema vipaumbele hivyo vimebainishwa kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2025/30 kwa lengo la kuwaleta wananchi maendeleo.
Dk Tulia ametoa matumaini hayo kwa wananchi wa kata ya Itezi leo Alhamisi Septemba 25, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni wa kunadi ilani ya uchaguzi na kuomba kura za mgombea urais, wabunge na madiwani.
Amesema anazitambua changamoto za maji na barabara tangu akiwa mbunge wa Mbeya Mjini, hata hivyo amewataka wananchi kuondoa mashaka kwani hilo lipo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
“Kwa sasa kuna visima viwili vya maji tumechimba ambavyo havikidhi mahitaji, tumeongea na wadau kwa ajili ya kuja na mradi wa kuchimba visima vikubwa lengo ni kuondoa tatizo lililopo na kuwatua akina mama ndoo kichwani,” amesema.
Amesema suala la barabara za mitaa, Serikali inaendelea kuboresha kwa kiwango la lami sambamba na ujenzi wa barabarani njia nne kutoka Nsalaga hadi Songwe na kusisitiza wananchi kwenda kutiki ifikapo Oktoba 29, 2025.
Amesisitiza Serikali imejipanga kutatua na kuondoa changamoto za wananchi katika nyanja mbalimbali na kwamba Jimbo la Uyole ni “kazi tu kwa vitendo”.
“Msiwe na hofu, Oktoba mkatiki, nafasi ya mgombea urais, wabunge na madiwani ili kufikiwa na maendeleo ndani ya siku 100 za Samia Suluhu Hassan alizosema mkoani hapa,” amesema mgombea huyo.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya kisasa na kujenga soko kubwa la kimataifa la mazao ndani ya viwanja vya maonyesho Nanenane,” amesema.
“Serikali imejipanga kwa ajili ya kazi, lakini pia suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi miaka mitano ijayo litawafikia wengi zaidi ili kuboresha kipato cha wajasiriamali wa mbogamboga na matunda,” amesema.
Awali, mgombea udiwani Kata ya Itezi, Angetile Kapolesya ameomba wananchi kutiki mafiga matatu kwa nafasi ya Rais, wabunge na madiwani ili kuleta chachu ya maendeleo.
“Kata hii changamoto kubwa ni maji, barabara za mitaa, ombi letu Dk Tulia, ukipata ridhaa tushike mkono kwani wananchi wanatambua mchango wako kabla hujawa mgombea wa jimbo hili la Uyole,” amesema.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Itezi wameitaka Serikali itupie kipaumbele kwenye suala la maji na mikopo asilimia 10 ili kuinua uchumi wa wajasiriamali wadogo.