Serikali yaonya utupaji wa plastiki baharini

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Usafiri wa Majini Duniani, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetawaka wananchi kupunguza uchafuzi wa plastiki katika bahari na kulinda rasilimali hiyo kwa vizazi vijavyo.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia Mazingira (UNEP), linaonyesha kila mwaka tani milioni 19 hadi 20 za plastiki zinatekezwa baharini, mtoni na kwenye maziwa.

UNEP inaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 85 ya taka zinazookotwa baharini ni plastiki, huku zaidi ya tani milioni nane za plastiki zikitupwa baharini kila mwaka duniani kote.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum  leo Septemba 25, 2025 kuhusu maadhimisho ya siku ya usafiri majini duniani, amesema siku ya leo inatoa fursa ya kipekee ya kutafakari, kutambua na kuthamini mchango muhimu wa sekta ya bahari katika kuunganisha dunia na kukuza biashara ya kimataifa kwa njia ya bahari.

“Katika miongo ya hivi karibuni, shughuli za binadamu zimeathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa bahari kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Uchafuzi wa plastiki, kemikali kutokana na kilimo na viwanda, kumwagika kwa mafuta, uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa hewa na uchimbaji wa madini baharini vimeleta athari kubwa kwa bahari na bioanuwai ya majini.


“Hivyo, wajibu wa kulinda bahari zetu unahitaji hatua za pamoja kutoka kwa watu binafsi, jamii na Serikali katika kushughulikia visababishi vikuu vya uchafuzi wa bahari,” taarifa hiyo imeeleza.

Salum kupitia taarifa hiyo amesema uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO₂) husababisha asidi baharini, hali inayokoleza athiri kwa viumbe vya majini.

Hali hiyo, amesema huchangia ongezeko la joto duniani ambalo husababisha kupanda kwa viwango vya maji ya bahari na kutishia maisha ya jamii nyingi za visiwa vidogo.

“Hivyo basi, hii ni fursa kubwa kwa nchi kuchukua hatua za kuhakikisha ulinzi wa uhai wa viumbe vya majini kwa kuunga mkono usafirishaji endelevu,” amesema Salum kupitia taarifa yake.

Salum amesema katika kuadhimisha siku ya leo ni  fursa kwa wananchi  kuhamasisha hatua stahiki kwa ajili ya ulinzi wa bahari kwa vizazi vijavyo na ustahimilivu wa sayari yetu, huku tukiendelea kutumia fursa za uchumi wa buluu.

Maadhimisho ya siku ya usafiri wa majini mwaka huu umeongozwa na kaulimbiu ya  “Bahari yetu, wajibu wetu, fursa yetu” ambayo kulingana na TASAC  inaikumbusha jamii umuhimu wa bahari na nafasi yake katika kuhifadhi na kusaidia uhai na bioanuwai ya viumbe wa majini,

Licha ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004  kuekeza wazi kuhusu wajibu wa wazalishaji katika kudhibiti taka wanazozalisha, ripoti ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inaonesha hadi tani milioni 20 za taka huzalishwa kila mwaka nchini.

Mtaalamu wa Masuala ya Mazingira, Dk Aidan Msafiri amesema ili kuboresha usalama wa usafiri wa baharini, mashirika ya kimataifa kama Shirika la Bahari Duniani (IMO) yameweka kanuni na viwango vya uendeshaji salama wa meli.

“Nchi zinapaswa kuhakikisha meli zina vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uokoaji, na mabaharia wanapatiwa mafunzo ya kutosha ya dharura.

Ushirikiano kati ya mataifa, uwekezaji katika teknolojia ya satelaiti, na utekelezaji madhubuti wa sheria ni nguzo muhimu za kulinda maisha ya wasafiri na mali baharini,” amesema.