Musoma. Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), inatarajia kutumia zaidi ya Sh13 bilioni kwenye ujenzi wa jengo la ofisi zake.
Hata hivyo, tayari mradi wa ujenzi huo kwa sasa umeshafikia asilimia 99 za utekelezaji wake.
Jengo hilo linalojengwa Mjini Kisumu nchini Kenya, litazinduliwa hivi karibuni na marais wa nchi nane za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Septemba 25, 2025 na Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo, Dk Masinde Bwire, fedha hizo ni michango kutoka Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dk Bwire amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu tatu ambapo tayari awamu mbili zimekamilika kwa asilimia 100 huku wakisubiri tarehe rasmi ya uzinduzi huo, ambayo itatangazwa na Rais wa Kenya, William Ruto ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la jumuiya hiyo.
“Awamu ya tatu inahusisha ujenzi wa maegesho ya magari pamoja na samani za ofisi na habari njema ni kwamba tayari makandarasi kwa ajili ya awamu hiyo wameshapatikana hivyo, wanatarajiwa kuanza kazi mara moja ambayo itakamilika ndani ya muda mfupi,” amesema.
Amefafanua kuwa kwa awamu ya kwanza na ya pili, wametumia zaidi ya Sh10.2 bilioni huku ikisemwa kwamba kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kuboresha zaidi shughuli zao tofauti na awali, shughuli za kamisheni hiyo zilikuwa zikifanyika katika ofisi walizopewa na Serikali ya Kenya.
Amesema fedha zilizotolewa na nchi hizo zimetumika kama ilivyotakiwa kwa maelezo kwamba inathamini michango hiyo iliyotokana na fedha za walipa kodi wa nchi za jumuiya hiyo.
“Tunafurahi kuwa sasa tuna nyumbani kwetu, sera za kisekta, kazi zetu na kila kitu kitafanyika na kuratibiwa kwenye hili jengo tunazishukuru nchi wanachama kwa hatua hii tuliyofikia, uwepo wa ofisi hii kutachangia utekelezaji wa shughuli zetu kwa ufanisi mkubwa na tija,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Musoma mkoani Mara wamesema kukamilika kwa jengo hilo kunatakiwa kwenda sambamba na utekelezaji wa shughuli za kamisheni hiyo kwa ufanisi na ubora.
“Nakumbuka kwenye maadhimisho ya siku ya Mara yaliyofanyika Butiama hivi karibuni kuna maagizo yaliyotolewa pale, sasa tunatamani kuona utekelezaji wake ukifanyika kwa kasi ya hali ya juu ili kunusuru mto Mara ambao upo katika hatari ya kutoweka,” amesema Elisha Mwita.
Katika maadhimisho ya siku ya Mara yaliyofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 12, 2025 pamoja na mambo mengine, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliiagiza Kamisheni hiyo kuanzisha jukwaa la wadau wa bonde la Mto Mara kwa ajili ya usimamizi na uendelevu wa mto huo.
Alisema miongoni mwa majukumu ya jukwaa hilo yatakuwa ni pamoja na kutafuta fedha kwaajili ya kugharamia shughuli za uhifadhi wa bonde hilo na miradi ya maendeleo rafiki kwa mazingira ya bonde la mto Mara.