Mabaharia wa Zenji waliamsha Afrika

MABAHARIA wa Zanzibar, KMKM inakuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kutupa karata katika mechi za marudiano ya michuano ya CAF wakati jioni ya leo itakapoikabili AS Port ya Djibouti kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.

KMKM ilianza vyema michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kushinda mabao 2-1 ikiwa wageni wa AS Port licha ya kwamba mechi ilipigwa hapohapo Amaan.

Matokeo hayo yameiweka pazuri mabaharia hao wakihitaji sare yoyote ili kutinga raundi ya pili na kusubiri kuvaana na mshindi wa mechi kati ya Azam FC na Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini na katika mechi ya awali iliyopigwa mjini Juba, Wanalambalamba walishinda 2-0.

Pambano hilo ambalo mashabiki wataingia bure kama njia ya kuwaongeza nguvu KMKM ili kumaliza kzi iliyopo mbele yao kabla ya nguvu hiyo kuelekezwa tena kesho Jumamosi wakati Mlandege inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika itakaporudiana na Insurance ya Ethiopia.

Katika mechi ya kwanza ugenini, Mlandege ilikung’utwa mabao 2-0 na hivyo kuwa na kazi ya kupata ushindi wa zaidi ya mabao 2-0 ili kutinga raundi hiyo ya pili na kuzika ile dhana klabu za Zanzibar huwa ni wasindikizaji katika michuano ya CAF.

Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali aliliambia Mwanaspoti, kikosi hicho kipo tayari kwa vita hiyo na AS Port wakiwa na kiu ya kuvuka raundi hiyo licha ya kwamba hawabweteki na matokeo ya mechi iliyopita waliocheza kama wapo ugenini.

“Katika mechi ya kwanza kuna vitu tumeviona kwa mpinzani wetu, tutajua namna ya kufanya marudiano ili kuhakikisha tunafuzu hatua inayofuata,” alisema Hababuu aliyekiri eneo la kiungo la kikosi hicho lilikuwa na changamoto kubwa aliyoifanyia kazi kuhakikisha inakuwa imara zaidi leo.

Kwa upande wa kocha wea Mlandege, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ akizungumza mechi yao ya kesho Jumamosi alisema, licha ya kupoteza mchezo wa ugenini, lakini bado wana matumani ya kupata matokeo mazuri nyumbani, huku akidai wapinzani wao sio timu tishio.

“Tumekutana na timu ya kawaida lakini imetuzidi kwa hali ya hewa yake, tunaamini katika mechi ijayo itakuja kulinda zaidi kwa sababu ina faida ya mabao mawili, upande wetu tutashambulia kwa lengo la kulazimisha matokeo,” alisema Baresi.

Mlandege inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao 3-0 ili kusonga mbele na kupta nafasio ya kuvaana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Pyramids ya Misri.

Kumekuwa na mzuka mwingi visiwani Zanzibar kutokana na hamasa nyingi zimetolewa na viongozi na wadau wa michezo, akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyeamua kulipa gharama zote za matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex na kuruhusu mashabiki kuingia bure.

Dk Mwinyi pia ametangaza kununua kila bao la mechi ya leo na kesho kwa Sh5 milioni, jambo linaloelezwa limewaongezea nguvu wachezaji wa KMKM na Mlandege zinazoshiriki pia Ligi Kuu ya visiwani hapa.