Historia inawabeba, Simba katika hili itavuka

KESHOKUTWA Jumapili, Simba itacheza mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Simba itakuwa chini ya kocha mkuu wa mpito, Hemed Morocco ambaye ameazimwa kutoka Taifa Stars ili ainoe Simba kutokana na changamoto ambayo imeikuta hivi sasa.

Hiyo inafuatia kuondoka kwa kocha mkuu wake Fadlu Davids na wasaidizi wake wanne ambao kwa sasa wapo Morocco wanakoitumikia Raja Casablanca.

Pia Selemani Matola ambaye pengine angeweza kusimamia timu katika mechi hiyo, alionyeshwa kadi nyekundu kule Botswana ambayo itamfanya atumikie adhabu ya kukosa mchezo mmoja.

Kuna watu wanaonyesha wasiwasi kwamba huenda Simba ikashindwa kufanya vizuri katika mchezo huo kutokana na hali iliyotokea na hivyo ikajikuta inashindwa kuvuka kuingia raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Hata hivyo, kijiwe kinaamini kwamba Simba itavuka kigingi cha Jumapili ikiwa chini ya Morocco kwani tayari viongozi wa timu hiyo na baadhi ya wachezaji wana uzoefu wa kukutana na changamoto kama iliyotokea na wakakabiliana nayo.

Waliwahi kuondokewa ghafla na Sven Vandenbroeck na bado waliweza kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pia waliwahi kuondokewa na Didier Gomes na bado wakacheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Na hata huyo Hemed Morocco ambaye wamemchukua, anao uzoefu wa kufundisha timu baada ya kuichukua kwa muda mfupi na ikaweza kufanya vizuri kinyume cha matarajio ya wengi.

Wote tunakumbuka katika fainali zilizopita za AFCON kule Ivory Coast, alibeba jukumu la kuinoa Taifa Stars baada ya Adel Amrouche kufungiwa na hakupoteza mechi mbili ambazo aliiongoza timu hiyo dhidi ya DR Congo na Zambia.