ZAIDI ya nyota 150 wa gofu kutoka mataifa sita ya kiafrika wanatarajia kushiriki michuano ya wazi ya Tanzania Open 2025, kuwania Sh35 milioni.
Nyota hao wanatoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Zimbabwe ambao wamethibitisha ushiriki wao zikiwa zimesalia siku saba kabla ya michuano hiyo itakayoanza Oktoba 2, kwenye viwanja vya Arusha Kili Golf.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga alisema michuano hiyo itakuwa ya siku nne ikishirikisha mashimo 72 na yatafikia tamati Oktoba 5, mwaka huu.
Kasiga alisema hadi kufikia juma hili kuna zaidi ya wacheza gofu 110 waliojiandikisha kwa ajili ya michuano hii huku wakitarajia wengine zaidi kushiriki.
“Tunategemea kupata washiriki 150 hadi kufikia tarehe ya kuanza michuano hii ya siku nne,” alifafanua Kasiga na kuongeza kiasi cha Sh35 milioni ndiyo kiwango cha zawadi za washindi wa michuano hii kwa gofu ya ridhaa na ya kulipwa na bingwa kwa wachezaji wa kulipwa ataondoka na Sh8.2 milioni na ridhaa atalipwa Sh2.5 milioni.