Vyoo vya kukaa raha, usasa lakini hatari

Katika enzi hii ya maendeleo ya kasi, ambapo miji inakua na teknolojia inachanja mbuga, vyoo vya kisasa vya kukaa vimeingia kwa kishindo katika nyumba nyingi za mijini.

Vinang’aa, vinaonekana vya kuvutia, na vinatoa hali ya starehe isiyo na kifani. Kwa hakika ni alama ya maisha ya kisasa yenye hadhi.

Hata hivyo, chini ya uso huo wa kung’aa, kuna simulizi ya tahadhari isiyojulikana na wengi.

Wataalamu wa afya wanaonya kuhusu madhara yanayoweza kutokana na matumizi ya vyoo hivi kwa muda mrefu na pasipo utunzaji sahihi.

Kimsingi, vyoo hivi vinaibuka kama tishio jipya, hasa katika jamii ambazo havikuanza kutumiwa kwa miongo mingi.

Kwa wengi, ni vigumu kuamini kuwa kitu kinachotoa faraja kama hicho kinaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya kiafya na kimazingira. Lakini ukweli unazidi kujitokeza: raha ya usasa huja na gharama yake.

Kwa karne nyingi, jamii barani Afrika na Asia zilikuwa zikitegemea vyoo vya kuchuchumaa.

Hata hivyo, maendeleo ya miundombinu, ustaarabu wa kimataifa, na kuongezeka kwa tabaka la kati mijini yamehamasisha matumizi ya vyoo vya kukaa.

Saimon Nyadwera, mtaalamu wa afya ya jamii, anasema vyoo vya kukaa ni suluhisho muhimu kwa makundi maalum.

“Ni vigumu kwa wazee, wajawazito, wagonjwa, na watu wenye ulemavu wa viungo kutumia vyoo vya kuchuchumaa. Vyoo vya kukaa huwapunguzia maumivu na kuwapa heshima ya kujihudumia bila msaada,” anasema.

Kwa nyumba za wageni, hoteli, na ofisi, vyoo hivi pia vinahusishwa na ustaarabu na hadhi.

“Vikitunzwa vizuri, hupunguza harufu na kusambaa kwa uchafu, na hutoa hisia ya usafi wa kisasa,” anaongeza  kusema.

Hali hii imewafanya watu wengi kuona vyoo vya kukaa kama alama ya maendeleo na maisha ya kisasa yenye starehe.

Pamoja na faida hizi, wataalamu wa afya wanatahadharisha kuwa vyoo vya kukaa, vinaweza kuwa chanzo cha magonjwa ikiwa havitatunzwa na kutumiwa kwa uangalifu.

“Kwa sababu ngozi inagusana moja kwa moja na kiti cha choo kinachotumika na watu wengi, uwezekano wa kuambukizwa bakteria, virusi, au fangasi ni mkubwa. Magonjwa ya njia ya mkojo (UTI), fangasi za ngozi, na maambukizi mengine yanaweza kusambazwa kwa urahisi.”anaeleza Dk Hamis Kulemba, daktari wa magonjwa ya binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu. 

Pia anaeleza kuwa hata mkao wa kukaa  katika vyoo hivyo una athari za kiafya.

“Ule mkao huongeza shinikizo kwenye njia ya haja kubwa, hali inayochangia bawasiri, kuzuia haja kutoka vizuri, na hata kuongeza muda unaokaa chooni, hasa kwa wale wanaopenda kutumia simu,”anaeleza.

Changamoto nyingine ni miundombinu. Vyoo vya kukaa vinahitaji maji ya kutosha na mfumo wa mabomba ulio bora, jambo ambalo halipatikani kwa urahisi vijijini au kwenye maeneo yenye uhaba wa maji. Hali hii inaweza kusababisha usafi hafifu na kugeuza choo kuwa kitovu cha maambukizi.

Utafiti wa mwaka 2021 uliochapishwa katika jarida la Antimicrobial Resistance & Infection Control Journal ulionyesha kuwa kuflashi vyoo vya kukaa husababisha chembe ndogo za maji  kurushwa hewani na kusambaza bakteria kama Klebsiella pneumoniae (CR-KP) katika mazingira ya hospitali.

Watafiti walipendekeza matumizi ya povu maalum inayowekwa kabla ya kutumia choo na kufunika kifuniko kabla ya ‘kuflashi’ ili kupunguza kuenea kwa vimelea.

Pia, mapitio ya kazi za kitafiti mwaka 2024 zilizokusanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Arizona nchini Marekani,  yanaeleza kuwa kuflashi vyoo vya kukaa,  kunasababisha moshi wa maji wenye vijidudu unaosambaa angani na kubaki hewani kwa muda mrefu.

Watafiti walihusisha hali hiyo na maambukizi kadhaa vikiwamo virusi vya Uviko, virusi vya magonjwa ya tumbo na matumbo na hata bakteria wanaaoleta maambukizi kwenye ngozi, mapafu na damu (MRSA).

Utafiti wa mwaka 2003 uliofanywa na Dk Dov Sikirov nchini Israel,  uligundua kuwa mkao wa kukaa kwenye vyoo vya kisasa huongeza shinikizo kwenye njia ya haja kubwa na huchukua muda mrefu kumaliza haja ikilinganishwa na mkao wa kuchuchumaa.

Watafiti walipendekeza kutumia stuli kuweka miguu juu ili kusaidia mwili kukaa kwenye mkao wa asili wa kutoa haja.

Ushuhuda kutoka kwa watumiaji

Mkazi wa jijini Mwanza, Zubeda Amos anaeleza changamoto alizokumbana nazo kutokana na kutumia vyoo vya kukaa kazini kwake.

“Nilikuwa na UTI mara kwa mara hadi nikapewa dozi ya sindano ili nipone. Nilihisi chanzo ni vyoo vya kukaa vya ofisini. Sasa nikitumia choo cha umma, nachuchumaa juu yake,” anasema.

Zubeda anashauri ofisi zijenge vyoo vya kuchuchumaa kwa watumiaji wa kawaida na kuwe na vyoo maalum vya kukaa kwa watu wenye ulemavu.

Dotto James, mkazi mwingine wa jijini Mwanza, anapendekeza  ofisi ziwe na vyoo vya aina yote kumpa mtumiaji chaguo.

“Ofisi nyingine zinakuwa na vyoo vya kukaa viwili na vya kuchuchumaa viwili. Hii inampa mtumiaji chaguo. Ni mfumo bora,” anasema.

Vipi wanaochuchumaa juu ya vyoo vya kukaa?

Ripoti ya Times of India (2025) inaonyesha wanawake wanaojisaidia kwa kuchuchumaa juu ya choo cha kukaa,  huongeza hatari ya majeraha ya misuli ya nyonga na UTI.

Katika ripoti hiyo, Dk Nikhil Khattar, mtaalamu wa mfumo wa mkojo,  anasema: “Kuchuchumaa juu ya choo huzuia utumbo kufunga vizuri, na hivyo kuacha mkojo kutokomaa kikamilifu. Hali hii huongeza hatari ya UTI, kuwasha kwa kibofu na matatizo ya muda mrefu”.

Wataalamu hao wanasema uoga wa uchafu kwenye vyoo vya umma huwasukuma wengi kuendelea kutumia mkao mbaya, na kwamba sio choo chenyewe kama  chanzo cha maambukizi.

Wataalamu wa afya wanashauri mtumiaji afunge kifuniko cha choo kabla ya ‘kuflashi’ ili kupunguza chembe za hewa.

Ushauri mwingine, safisha kiti cha choo kwa dawa za kuua vimelea kabla ya kukaa, kuepuka kutumia simu chooni ili kupunguza muda wa kukaa na shinikizo kwenye mishipa ya haja kubwa.

Pia, kaa kwa usahihi, epuka kuchuchumaa juu ya sahani ya choo cha kukaa, kwani  mkao wa kuchuchumaa juu yake unaweza kusababisha maumivu na UTI.