Bado Watatu – 40 | Mwanaspoti

TUKATOKA pale kituoni na tukachangukana. Mimi na Sufiani tulikodi bajaj tukaenda nyumbani. Kwa vile sote tulikuwa na makosa, hakukuwa na yeyote aliyemlaumu mwenzake.
Siku iliyofuata tulikwenda kuandikisha maelezo yetu na hatimaye Raisa alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuua. Wakati Raisa anafikishwa mahakamani, mimi na Sufiani tulikuwa tumeshaachana kutokana na tukio hilo. Hatukuwa tukiaminiana tena.
Hapo ndipo nilipoamua kubadili jina langu na kuitwa Hamisa, baada ya kuona jina la Rukia lilikuwa na mikosi mingi.
Huo ndio mkasa alionieleza Hamisa. Kwa kweli ulinisisimua sana. Nilimpa pole na nikamtaka asirudie tena vitendo vya aina hiyo.
Uhusiano yetu ulianza mara tu alipopata kazi ya uuguzi aliyokuwa ameusomea baada ya kumaliza sekondari. Hii ilikuwa baada ya saluni yake kufilisika.

Kuanzia siku hiyo tukawa wapenzi mimi na Hamisa. Hamisa alifanikiwa kuharibu akili yangu nikawa kama zezeta. Kama ningekuwa mshirikina, ningeamini alinilisha limbwata.
Lakini ukweli ni kuwa hakunilisha limbwata la uchawi, bali alinilisha limbwata la penzi adhimu alilokuwa akinipa.
Tukapanga uchumba, lakini ukaja kuharibika ghafla baada ya Hamisa kurushiwa video ikinionyesha nikicheza na msichana mmoja nikiwa mlevi, huku nikimshika sehemu zisizostahili.
Hamisa alichukulia kuwa yule msichana alikuwa mpenzi wangu, hivyo akaamua kuvunja uchumba wetu.
Siku ile nilipokuwa ninawaza haya, ndipo nilimpigia simu na akanijibu kuwa anamuhudumia mgonjwa.
Nikiwa katika furaha ya kupata jibu lake ndipo nilipokumbuka tulivyoanzana mimi na yeye mpaka tukawa katika uhusiano huo.
Mida ya saa tano usiku nilimpigia Hamisa, nikiwa najua ameshatoka kazini. Wakati huo nilikuwa sebuleni kwangu nikitazama televisheni.
Hamisa alichukua muda kidogo kupokea simu. Alisema:
“Hello!”
Sauti yake ilikuwa nzito, ikionyesha kuwa nilimuamsha usingizini.
“Umelala?” nikamuuliza.
“Nilikuwa nimepitiwa na usingizi…” Hamisa akajibu.
“Samahani. Nilikupigia muda huu kwa kuhisi kuwa umeshatoka kazini.”
“Bila samahani. Nililala ghafla tu, sijazima televisheni wala taa… Kwema huko?”
“Huku ni kwema, sijui kwako?”
“Nashukuru…”
Nikamsikia Hamisa akipiga miayo, kisha akaniuliza:
“Ulikuwa unasemaje?”
“Nilitaka kukusalimia tu Hamisa. Umekuwa kimya sana.”
“Kwani umesahau nini kimetokea?”
“Hakuna kilichotokea isipokuwa mawazo yako tu, Hamisa. Unanituhumu bure.”
“Una maana kuwa Helena si mpenzi wako?”
“Kweli kabisa. Sina mawasiliano na Helena.”
“Hapo ndipo unaponikwaza. Huna uhusiano na msichana ambaye mnacheza naye muziki na kushikana mkionekana wazi kama wapenzi?”
“Kusema kweli, labda ni hali ya ulevi tu. Lakini mimi na Helena si wapenzi. Sasa kama hiyo video ndiyo iliyokuudhi, nisamehe.”
“Acha nifanye utafiti. Nikiridhika kwamba wewe na Helena si wapenzi nitakufahamisha.”
“Huo utafiti wako utachukua muda gani?”
“Sijui.”
“Kwa hiyo unaweza kuchukua hata mwezi?”
“Hata mwaka. Nataka nijiridhishe kabisa.”
“Hata mwaka! Hamisa, acha mzaha! Unajua tangu ukate mawasiliano na mimi nimechanganyikiwa.”
“Ukichanganyikiwa ndio utatia akili. Acha nifanye utafiti wangu kwa muda ninaotaka.”
“Kwa hilo sikubaliani na wewe. Niambie angalau nikupe wiki moja.”
“Wiki moja ndogo sana.”
“Basi wiki mbili.”
“Kwani wewe una wasiwasi gani?”
“Na kwanini nisiwe na wasiwasi wakati sikuelewi Hamisa?”
“Utanielewa tu. Naomba unisubiri.”
“Sawa. Kwa vile nakuhitaji nitakuwa na subira.”
“Si unajua subira huvuta heri?”
“Ninajua.”
“Basi subiri.”
“Hakuna shaka.”
“Acha nizime taa nilale.”
“Sawa. Usiku mwema.”
“Na kwako.”
Nikakata simu. Ingawa majibu ya Hamisa hayakuwa mazuri sana, lakini yalinipa moyo. Nilijua mwanamke yeyote haachi kuringa. Kumzungusha mwanaume ni sehemu ya maringo yake. Niliamini Hamisa angerudi mikononi mwangu kwani tayari alikuwa ameshaonyesha kulegea.
Usiku ule nililala usingizi mzuri na kupata ndoto njema.
Siku iliyofuata saa tano asubuhi, afisa upelelezi alinipigia simu na kuniita ofisini kwake.
Aliponiona, alinipa hati ya mahakama iliyotoa ruhusa ya kufukua makaburi ya wafungwa wanne waliotakiwa kufanyiwa uchunguzi.
Tukumbuke sasa hivi tuko katika ile hadithi tuliyoanza nayo kuhusu watu waliokuwa wakinyongwa.
“Tutakwenda pamoja na wataalamu wa kutambua vinasaba,” afisa upelelezi akaniambia.
Saa saba mchana tukawa katika ofisi ya mkuu wa gereza la Maweni. Tulikuwa mimi, afisa wangu na makachero watatu wa chini yangu. Pia tulikuwa na wataalamu wawili kutoka hospitali ya Bombo.
Nilimpa mkuu wa gereza hati ya mahakama iliyotoa ruhusa ya kufukua makaburi ya wafungwa wanne walionyongwa.
Mkuu wa gereza baada ya kusoma kibali hicho alisema:
“Hiki kibali ni muhimu kwa sababu haya makaburi yako mikononi mwa serikali. Ni lazima tufuate taratibu. Sasa ni ruksa kuyafukua.”
Tukatoka ofisini kwake na kuelekea eneo la makaburi ya wafungwa walionyongwa. Kulikuwa na takriban makaburi kumi na manane, mengine yakiwa ya tangu enzi za ukoloni.
Kila kaburi lilikuwa na jina la mfungwa, tarehe aliyonyongwa na kuzikwa.
Mkuu wa gereza na maafisa wake walituonyesha makaburi tuliyoyataka. Tukapewa mashepe, kisha makachero wetu wakaanza kufukua kaburi moja baada ya jingine.
Kaburi la kwanza lilikuwa la Ramadhani Unyeke au John Lazaro.
Baada ya kulifukua, tuliupata mwili wake ambao tayari ulikuwa umeharibika. Mwili ulipigwa picha na kuchukuliwa alama mbali mbali kwa uchunguzi, kwani haukuweza kutambulika kwa sura.
Baada ya kumaliza kazi, kaburi hilo lilifukiwa tena na tukafukua jingine. Tuliendelea hivyo hadi kumaliza yote manne.
Sasa kazi ilikuwa kupeleka sampuli za vinasaba na alama mbalimbali kwa wataalamu. Lakini nilijiuliza: Ile miili ya kina Unyeke tuliyoiona mochwari ilikuwa ya nani, wakati sasa tumewakuta kaburini?
Hadi saa kumi jioni tulikuwa tumesharudi ofisini. Uchunguzi wa sampuli tuliwaachia wataalamu.
Mimi nilikwenda nyumbani kupumzika. Nilifikiria kumpigia Hamisa lakini nikahisi atakuwa kazini, hivyo nikaacha.
Saa saba mchana ya siku iliyofuata tulipokea matokeo ya uchunguzi wa picha, alama za vidole na vinasaba.
Matokeo yalionyesha kuwa miili ile haikuhusiana kabisa na kina Unyeke. Tafsiri yake ni kwamba waliokuwapo kaburini walikuwa watu wengine, lakini walizikwa kwa majina ya kina Unyeke.
Hali hiyo ilitupa taharuki polisi kwa kuhisi kulikuwa na udanganyifu mkubwa.
Mimi na afisa upelelezi tulikwenda kumuona tena mkuu wa gereza saa tisa alasiri.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa watu waliohukumiwa kunyongwa siyo walionyongwa wala kuzikwa kwenye makaburi yale,” afisa upelelezi akasema.
Mkuu wa gereza alishituka:
“Unasemaje?”
Afisa upelelezi akarudia maelezo, lakini mkuu wa gereza akatikisa kichwa.
“Haiwezekani kufanyika udanganyifu kama huo.”
“Lakini uchunguzi wa vinasaba na alama za vidole ndio umeonyesha hivyo.”
“Tangu nianze kazi sijawahi kusikia jambo kama hili. Lakini kwa kuwa wakati huo mimi sikuwapo hapa, siwezi kulizungumzia.”
“Umeanza lini hapa?”
“Nina miezi sita tu. Nilihamishwa kutoka gereza la Ukonga.”
“Kwa hiyo wakati unakuja, hao wafungwa walikuwa wameshanyongwa tayari?”
“Ndio.”
“Na kabla yako alikuwapo nani?”
“Kabla yangu alikuwapo Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mzee Hashim Malick.”
“Hivyo watu hao walinyongwa chini ya uongozi wake?”
“Ndiyo, kwa sababu yeye ndiye alisaini hati za kunyonga.”
“Alipoondoka alikwenda wapi?”
“Kwa sasa amestaafu.”
“Alistaafu lini?”
“Baada ya kustaafu kwake ndipo mimi nikaletwa hapa.”
“Yuko wapi hivi sasa?”
“Kwa bahati nzuri yupo hapa Tanga, ni mwenyeji wa Mwambani.”
“Tupatie anuani yake.”
“Nina namba yake ya simu, nitakupatia.”
Mkuu wa gereza akachukua kitabu cha namba, akatafuta namba ya Hashim Malick na kuisoma. Afisa upelelezi akaandika kwenye simu yake.
Kisha akamuuliza tena:
“Baada ya kushika uongozi wa gereza, hujawahi kugundua mabadiliko yoyote ya idadi ya waliofungwa au kunyongwa?”
“Hapana, sijagundua chochote. Hili la leo ndilo limenishitua.”
“Kwa hiyo hujagundua kuna wafungwa waliotakiwa wanyongwe lakini hawakunyongwa?”
“Sijawahi kugundua. Nafikiri mstaafu Hashim Malick ndiye mwenye maelezo.”
“Sawa.”
Tulipokuwa tukirudi mjini, afisa wangu akasema:
“Ninaamini Hashim Malick anajua alichokifanya.”
“Na si rahisi mtu mwingine kukijua.”
“Ni lazima apatikane atueleze, maana yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa gereza.”
Tulifika ofisini kwa afisa upelelezi, naye akampigia simu Hashim Malick. Simu iliita kwa muda mrefu, hatimaye ikapokewa.