Coastal Union tatizo lipo hapa tu!

BAADA ya kukusanya pointi tatu na mabao mawili katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara, Kocha wa Coastal Union, Ally Ameir amesema licha ya kuwa na kikosi kizuri, tatizo lipo eneo la ushambuliaji na anatumia muda uliosalia kurekebisha tatizo kabla ya kuvaana na Dodoma Jiji.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mwaka 1988 ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa JKT Tanzania mechi zote ikicheza Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga na sasa inajiandaa kuifuata Dodoma ugenini.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Ameir alisema anafurahishwa na uwezo mkubwa wa wachezaji waliouonyesha katika mechi zilizopita ikiwamo waliodondosha pointi tatu na kilichowaponza ni umakini mdogo eneo la ushambuliaji na ndipo anapokomalia kwa sasa kabla ya kuifuata Dodoma.

“Timu yangu inacheza vizuri, nimekaa nayo muda mfupi tukipata nafasi ya kutengeneza muunganiko kwa kucheza mechi za kirafiki nimeshuhudia mabadiliko makubwa yanayoleta tija katika mechi ya kwanza na hata ya pili, japo tulipoteza,” alisema kocha uyo kutoka Zanzibar na kuongeza;

“Nimebaini upungufu katika safu ya ushambuliaji, ninachotaka kukifanya ni kuwajenga washambuliaji wangu kukaa kwenye nafasi na kutumia nafasi wanazotengeneza ili kujiweka kwenye nafasi nzuri hasa mzunguko huu ambao ndio unatoa picha ya timu itavuna nini mwisho wa msimu.”

Ameir alisema kesho Jumamosi Coastal itakuwa ugenini kukabiliana na Dodoma Jiji na  anatambua hautakuwa mchezo rahisi lakini anaandaa timu yake ambayo itatoa upinzani na hatimaye kukusanya pointi tatu na kurudi kwenye mstari baada ya kudondosha pointi nyumbani.

“Ligi imetoa picha ni namna gani unatakiwa kujipanga ili uweze kuwa mshindani mechi mbili tulizocheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani zimetuwashia taa kujua ni namna gani wapinzani pia wamejipanga hatupo tayari kuwa wanyunge kwa kugawa pointi kwa wapinzani tunaendelea kujifua kushindana.”