Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Dar es Salaam, imetoa taarifa kuhusu shauri la madai ya ardhi lililofunguliwa na mjane, Alice Haule, kuhusu mgogoro wa nyumba.
Septemba 23, 2025 kupitia vyombo vya habari Alice alizungumzia kuhusu uwepo wa shauri hilo kwenye mahakama hiyo, baada ya nyumba yake kuvamiwa na watu waliotoa vitu nje kwa nguvu.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Septemba 25, 2025, mahakama hiyo imezungumzia shauri hilo kuhusu umiliki wa nyumba iliyopo kiwanja namba 819, chenye hati namba 49298, eneo la Msasani Beach, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Gerard Chami, Mkuu wa kitengo cha habari, elimu na mawasiliano imesema shauri husika lilifunguliwa Februari 11, 2025 na Alice Haule, ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu Justice Rugaibula, aliyefariki dunia Septemba 25, 2022.
“Shauri hilo, lenye namba 3143/2025 liliwasilishwa kupitia Wakili Mwesigwa Muhingo katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, dhidi ya Mohamedi Mustafa Yusufali, Kamishna wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikidaiwa kuwa nyumba tajwa ni mali ya marehemu,” inaeleza taarifa hiyo.
Imeelezwa baada ya kupitia hatua za awali za usikilizwaji wa shauri ikiwa ni pamoja na uwasilishaji wa nyaraka za wadaawa wote katika shauri na kufanyika usuluhushi ambao ni takwa la kisheria, shauri lilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa kongamano la mwisho Septemba 19, 2025.
“Siku hiyo, wakili wa Alice, Mwesigwa Muhingo, aliomba kuliondoa shauri hilo kwa ruhusa ya kulifungua upya ili kumuongeza Msajili wa Hati kama mdaiwa. Mahakama ilikubaliana na maombi ya wakili wa Alice na shauri hilo namba 3143 la mwaka 2025 liliondolewa kwa ruhusa ya kulirudisha tena,” imeelezwa.
Taarifa inaeleza Septemba 19, wakili Muhingo aliwasilisha upya maombi ya kufungua shauri la madai ya ardhi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.
“Hata hivyo, hati ya madai aliyowasilisha ilikuwa na mapungufu ya kisheria, hivyo maombi yake hayakusajiliwa na aliagizwa kufanya marekebisho,” imeelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kurekebisha hati ya madai, Septemba 24, shauri lilisajiliwa na kupewa namba 24396/2025 likiwa na marekebisho aliyoyaomba ya kumuongeza Msajili wa Hati kama mdaiwa.
“Leo (jana) Septemba 25, 2025 Alice amewasilisha maombi madogo namba 24541/2025 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, akiomba zuio la muda la kutoondolewa kwenye nyumba iliyopo kiwanja namba 819, chenye hati namba 49298, Msasani Beach, Dar es Salaam,” inaeleza taarifa na kuongeza:
“Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili Mkuu wa Mahakama, tunaomba umma utambue kuwa mashauri yote mawili yako katika hatua mbalimbali mahakamani.”