Simba yalia na mashabiki, yafafanua adhabu ya CAF

Wakati ikijiandaa kucheza bila mashabiki katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, Jumapili, Septemba, 29, 2025 na faini ya Dola 50,000 (Sh123 milioni), Simba imekutana na adhabu mpya kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Adhabu hiyo mpya ni ya faini ya Dola 30,000 (Sh74 milioni) kutokana na makosa ambayo ilifanya katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, Mei 25, mwaka huu.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amethibitisha hilo leo Ijumaa Septemba 26, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwaasa mashabiki kutofanya vitendo vinavyoigharimu tena klabu hiyo.

“Hasara ya kwanza tunakosa mashabiki, hasara ya pili tunakosa mapato na hasara ya tatu tunalipa faini ya Dola 50,000. Vilevile tumepewa adhabu kutokana na mechi ya fainali dhidi ya RS Berkane, vilevile tuliwasha fireworks.

“Kwenye mechi ya fainali tumetozwa faini ya Dola 35,000. Jumla Tumetozwa Dola 85,000 sawa na Sh200 milioni.

“Tunacheza bila mashabiki kwenye mechi dhidi ya Gaborone United pekee lakini sababu tumefanya makosa mfululizo CAF watakuwa makini na sisi kwelikweli sababu wanaona tunafanya vitendo ambavyo sio vya kiungwana hivyo watakuwa wanaangalia kama Simba Sports Club tumebadilika. Ni lazima tuwe makini kwelikweli ili kuwaonyesha kwamba tumejifunza na tumebadilika. Kuanzia hivi sasa tuchukue taswira mpya kwenye eneo la ushabiki,” amesema Ahmed Ally.

Ahmed Ally amesema kuwa klabu itaendesha zoezi la mchango kwa mashabiki ili kupunguza mzigo wa deni hilo.

“Wapo mashabiki ambao wametaka kuwa sehemu ya maumivu ambayo tunapitia Klabu ya Simba na maumivu yenyewe ni faini ya Tsh. 212,500,000 sawa na Dola 85,000.

“Kwa mapenzi yao mashabiki wameomba kuchangia faini ili kuipunguzia klabu mzigo na sisi tumepokea na tumeridhia mashabiki wachangie hususani kwenye eneo la faini.

“Niwaase mashabiki wenzangu wa Simba, tuache vitendo vya vurugu uwanjani. Kwanza tuanze ulinzi wa wenyewe kwa wenyewe ukiona mtu anataka kuwasha zile fireworks muie, ukiona mtu anataka kuingia uwanjani tushirikiane kumzuia ikiwezekana kumtoa uwanjani. Angalia mechi kama hii tunakwenda uwanjani bila mashabiki. Hatupo hapa kulaumiana ila kukumbushana,” amesema Ahmed Ally. Katika mchezo dhidi ya Gaborone United, Simba inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

Wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wanaingia wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza ugenini huko Botswana wiki iliyopita.