SIMBA inajiandaa kushuka uwanjani keshokutwa dhidi ya Gaborone United ya Botswana katika pambano la marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila mashabiki kutokana na adhabu iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Simba imeadhibiwa na CAF kutokana na matukio ya fujo zilizofanywa kwenye mechi za msimu uliopita za Kombe la Shirikisho Afrika ikitakiwa kulipwa faini ya zaidi ya Dola 85,000 (takriban Sh212 milioni) sambamba na kuzuiwa kuingiza mashabiki katika pambano la Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally amesema kutokana na vurugu zilizofanywa na mashabiki katika mechi dhidi ya Al Masry ya Misri na ile ya RS Berkane ndizo zimewafikisha hapo.
Ahmed amesema adhabu hiyo iliyotokana na kuwasha fataki na vurugu katika viwanja viwili ambavyo Simba ilicheza mechi hizo vya Mkapa na New Amaan zimeigharimu adhabu ya faini ya Dola 85,000.
“Adhabu zimetokana aina mbili ya kwanza ni mashabiki kutokuingia mashabiki katika mechi ijayo, pili faini ya Dola 85,000 ambazo pia ziko kwenye makosa mawili. Dola 50,000 ni kwa makosa ya vurugu katika mechi ya kwanza robo fainali na Dola 35,000 katika fainali dhidi ya RSC Berkane, kule Zanzibar.
MASHABIKI WALIPA
Ahmed amesema wapo mashabiki walioamua kubeba mzigo kwa kulipa faini ambazo.
“Mashabiki baadhi waliomba wachangie deni hilo na sisi bila hiana tukaona tuwaunge mkono kwa kukubali jambo hilo lifanyike kwa mapenzi waliyonayo na klabu,” amesema Ahmed.
JUMAPILI WOTE HAPA
Ahmed ameizungumzia mechi ya marudiano na Gaborone akisema: “Siku ya Jumapili wote tukutane pale Mwembeyanga kwa ajili ya kuangalia mechi kwa pamoja na tutaanza kama kawaida.
“Kama ilivyokuwa mechi dhidi ya Constantine, ila haizuii kupata raha au kukutana kama inavyokuwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.”
WAAMUZI
Ahmed amewataja waamuzi wa pambano hilo kuwa wote wanatokea Niger.
“Waamuzi wote ni kutoka Niger na walikuwa njiani kuja nchini. Katikati atakuwa Mohamed Ally Mussa, huku wasaidizi namba moja ni Abubakary Athuman wakati namba mbili ni Abdullah Adal na wa mezani atakuwa ni Moussa Ahmadou.
Simba inacheza mechi hiyo ya nyumbani ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata ugenini wikiendi iliyopita na kesho itahitaji sare ya aina yoyote au kushinda ili itinge raundi ya pili ya michuano hiyo waliyoirejea baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu.