New York. Upatikanaji wa taifa huru la Palestina umebakiza ngazi moja, baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha kwa kura nyingi ‘Azimio la New York’ linalofufua suluhisho la mgogoro wa mataifa mawili – Israel na Palestina.
Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933, ndio unaelekeza vigezo vya kutambua taifa huru chini ya sheria ya kimataifa.
Vigezi hivyo ni taifa husika kuungwa mkono na nchi tisa ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo hadi sasa ndani ya baraza hilo Palestina imeungwa mkono na mataifa 11, zikiwamo nchi nne zenye kura ya veto.
Pia, katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ili taifa la Palestina litangazwe kuwa huru, inahitajika theluthi mbili ya nchi wanachama 193, sawa na nchi 128 na tayari imepata kura 142.
Azimio hilo la New York, limepitishwa na mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likihimiza suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina lililofikiwa mwaka 1967, ikiwamo kuweka mipaka ya kinchi.
Novemba 22, 1967, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 242, kufuatia vita vya siku sita kati ya Israel na Palestina, kuanzisha mataifa mawili. Hata hivyo, utekelezaji wa azimio hilo ulianzisha taifa moja la Israel.
Tamko la New York hilo lililopitishwa mwanzoni mwa mkutano huo ni matokeo ya mkutano uliotishwa na nchi za Ufaransa na Saudi Arabia kujadili umuhimu wa kutambua taifa la Palestina kwa lengo la kumaliza vita eneo la Mashariki ya Kati.
Mkutano wa Baraza Kuu unaojumuisha nchi wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa, nchi 142 zilipiga kura kuunga mkono ‘Tamko la New York’ hilo ili kuwa azimio, nchi 10 zilipinga na kura 12 hazikuwa na upande wowote.
Israel ilipinga azimio hilo, pamoja na nchi tisa zikiwamo Argentina, Hungary, Micronesia, Nauru, Palau, Papua New Guinea, Paraguay, Tonga na Marekani.
Sehemu ya utangulizi wa azimio hilo inarejelea kutokubalika kwa kuchukua ardhi kwa njia ya vita na umuhimu wa kufanya kazi kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu katika Mashariki ya Kati, ambapo kila Taifa katika eneo hilo linaweza kuishi kwa usalama.
Aya ya kwanza ya utekelezaji ya azimio hilo Inathibitisha kwamba kutekelezwa kwa kanuni za Katiba kunahitaji kuanzishwa kwa amani ya haki na ya kudumu katika Mashariki ya Kati
Pia, azimio hilo lenye kurasa saba limetoa wito wa hatua ya pamoja ya kumaliza vita vya Gaza, na kufikia suluhisho la haki, amani na la kudumu la mzozo wa Israel na Palestina kulingana na utekelezaji wa dhati wa suluhisho la Mataifa Mawili.
Pia, azimio hilo linata kundi la Kipalestina la Hamas, linaloongoza serikali ya Gaza, kuwaachilia mateka wote, na kuagiza kwamba “likome kutawala Gaza na likabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina kwa lengo la kuundwa kwa taifa huru la Palestina na lenye mamlaka kamili.
Kabla ya kura kupigwa, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Jérôme Bonnafont alikumbusha kuwa Azimio la New York linaweka ramani ya kufanikisha suluhisho la mataifa mawili.
Bonnafont alisema ramani hiyo inahusisha kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na kuanzishwa kwa Taifa la Palestina lenye uwezo wa kujiendesha na uhuru kamili.
Ramani hiyo pia inataka Hamas wasalimishe silaha na wajiondoe kwenye mamlaka ya kuongoza Gaza, kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Israel na nchi za Kiarabu, pamoja na dhamana za usalama wa pamoja.
Akizungumza kabla ya kura kupigwa, Balozi wa Israel Danny Danon alisema kwamba azimio hili lenye upendeleo wa upande mmoja halitakumbukwa kama hatua kuelekea amani, bali kama ishara nyingine isiyo na maana inayodhoofisha uaminifu wa mkutano wa Baraza Kuu.
Alisema kuwa Hamas ndilo mshindi mkubwa wa kuidhinishwa kwa jambo lolote hapa na kwamba wataita matokeo hayo ‘matunda ya Oktoba 7, 2023’.
Oktoba 7, 2023, Hamas lilishambulia Israel, na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka watu 251, hali iliyozusha mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika Gaza, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya Wapalestina.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alieleza kuwa “swali kuu kuhusu amani ya Mashariki ya Kati ni utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili, ambapo mataifa mawili huru, yenye mamlaka kamili na kidemokrasia ya Israel na Palestina wanaishi kwa amani na usalama kandokando.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.