Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amewasihi Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kuipigia kura CCM ili kukipa chama hicho ushindi wa heshima.
Ikiwa umebaki mwezi mmoja kuelekea uchaguzi mkuu, Rais Samia ameweka alama nyingi katika uongozi wake ambazo zinatarajiwa kuwa turufu kubwa kwake kuzoa kura za urais na kuibuka mshindi.
Samia, ambaye aliapishwa kama Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 19 Machi 2021, ameweka historia kama kiongozi wa kwanza mwanamke kushika nafasi hiyo nchini.
Katika muhula wake wa kwanza wa miaka minne, amefikia mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi, diplomasia, haki za binadamu, na maendeleo ya miundombinu.
Hapa chini ni muhtasari wa baadhi ya mafanikio yake makubwa matano ambayo yatambeba kushinda uchaguzi wa rais kwa ushindi wa heshima:
1. Uongozi wa Uchumi na Ukuaji wa Pato la Taifa
Uchumi wa Tanzania umekua kwa kasi chini ya uongozi wake, kutoka dola bilioni 69.7 mwaka 2021 hadi makadirio ya dola bilioni 86 mwaka 2025, na ukuaji wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka. Amedhibiti mfumko wa bei hadi asilimia 4.4 na kupunguza umaskini hadi asilimia 26.6. Pia, amesaini mikataba ya uwekezaji yenye thamani zaidi ya dola bilioni 2, na kuimarisha sekta za madini na nishati.
2. Maendeleo ya Miundombinu
Rais Samia amekamilisha miradi mikubwa kama Daraja la Kigongo–Busisi (John Pombe Magufuli Bridge), ambalo ni la pili kwa urefu Afrika Mashariki. Pia, amepata mkopo wa mradi wa mwendokasi BRT (Bus Rapid Transit) na kuimarisha barabara, reli ya SGR, bwawa la umeme la JNHPP, vivuko, ununuzi wa ndege za ATCL na ujenzi wa viwanja vya ndege, ambapo alipokea Tuzo la Babacar N’Diaye kwa bidii yake katika maendeleo ya barabara mwaka 2022.
3. Kuimarika kwa sekta ya Afya
Mara baada ya kuapishwa kuwa Rais, Samia alikabiliana na janga la Uviko-19 kwa umahiri mkubwa na kufikia lengo la chanjo asilimia 50 kwa takriban watu milioni 30 wa Tanzania. Ametangaza bima ya afya kwa wote, kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa maskini, na kuajiri madaktari na watahini 5,000. Pia, amepiga marufuku hospitali kushikilia miili ya marehemu kwa madeni. Serikali yake imefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 80% (kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi 100,000) na vifo vya watoto chini ya miaka 5 kwa asilimia 33% (kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi 1,000) ndani ya muongo mmoja. Hii imesababisha Rais Samia kupokea Tuzo ya Global Goalkeeper Award kutoka Taasisi ya Gates Foundation mnamo Februari 2025, kwa mafanikio katika afya ya mama, mtoto na lishe. Serikali yake imejenga hospitali mpya 129 katika wilaya zote nchini, na kuimarisha huduma za afya za mama na watoto.
4. Mageuzi ya Elimu
Katika miaka miwili ya kwanza ya utawala wake (2021–2023), serikali imejenga zaidi ya vyumba vya madarasa 20,000 katika shule za msingi na sekondari kote nchini, ikijumuisha vyumba 3,000 katika shule za shikizi (sekondari) 970. Serikali imefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, na maabara za sayansi katika shule za sekondari.
Zaidi ya wanafunzi 19,264 wamepata fursa ya mafunzo katika sekta sita za kipaumbele kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Jamii (SDF), ili kuwapa ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa.
5. Mapinduzi ya Kilimo
Sekta ya kilimo imekuwa kipaumbele cha Rais Samia, ambapo bajeti imeongezeka mara nne katika miaka mitatu, ili kuimarisha uzalishaji, masoko na miundombinu. Hii imenufaisha wakulima wengi, hasa vijijini.
Mpango wa Tanzania Mercantile Exchange (TMX) umepunguza wizi wa mazao na kutoa bei bora kwa wakulima kupitia simu.
Miundombinu na teknolojia: Ujenzi wa Maabara Kuu ya Kilimo Dodoma umezinduliwa mnamo Agosti 2025 ili kuhakikisha usalama wa chakula na kuvutia wauzaji wa nje. Pia, miundombinu ya umwagiliaji imerejeshwa ili kufanya kilimo cha kudumu, na kuongeza bajeti ya kilimo kwa asilimia 300 ili kupunguza gharama na kuongeza tija.