Ecobank Tanzania Yazindua Toleo Jipya la ‘Ellevate’ kwa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake

 Ecobank Tanzania imezindua rasmi toleo lililoboreshwa la mpango wake wa “Ellevate by Ecobank”, likiwa na lengo la kuharakisha ujumuishaji wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake wajasiriamali..

Awali, Ellevate ilianzishwa kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) zinazoongozwa au kumilikiwa na wanawake. Hata hivyo, mpango huu sasa umeboreshwa na kupanuliwa ili kuwafikia wanawake katika sekta zote za biashara kuanzia makampuni makubwa, SMEs hadi wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu, alisema mpango huu umekuwa na mchango mkubwa kwa wafanyabiashara wanawake nchini.

“Wafanyabiashara wanawake wa Tanzania tayari wameshuhudia manufaa ya ‘Ellevate by Ecobank’. Tangu kuanzishwa kwake, tumewasaidia zaidi ya wanawake wajasiriamali 300. Toleo hili jipya linaimarisha dhamira yetu ya kuwa benki ya chaguo kwa wanawake wajasiriamali na kuendeleza nafasi yetu katika kusukuma mbele ujumuishaji wa kifedha barani Afrika,” alisema Dkt. Asiedu.

Aliongeza kuwa kupitia Ellevate, wanawake wa Afrika watapata huduma za kifedha za viwango vya kimataifa, zinazowawezesha kuongeza ukuaji wa biashara zao, kupata faida endelevu na kujiimarisha kwa muda mrefu.

Pia amesema miongoni mwa faida zinazotolewa kupitia mpango huu ni pamoja na mikopo isiyo na dhamana hadi kufikia Dola za Kimarekani 50,000, kupunguzwa kwa vikwazo vya kuingia kwenye mpango kwa historia ya miaka miwili ya biashara pekee badala ya mitatu, pamoja na masharti nafuu ya dhamana na viwango vya riba vinavyoshindana.

“Wanawake wajasiriamali watanufaika na fursa za kupanua masoko kupitia jukwaa la MyTradeHub linalowaunganisha na wateja wapya barani Afrika, pamoja na mafunzo ya kukuza uwezo wa biashara na uongozi, na upatikanaji wa huduma za bima, usimamizi wa mali na ulinzi wa mishahara.” Alisema Dkt. Asiedu.

Kwa uzinduzi huu, Ecobank Tanzania inaendelea kuwa kinara katika kuhimiza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kupata nyenzo, maarifa na mitaji itakayowawezesha kustawi katika biashara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Charles Asiedu akizungumza na Wanawake Wajasiriamali wadogo, wakati na wakubwa wakati wa kufungua semina ya mpango maalum ujulikanao kama ‘Ellevate by Ecobank’ iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Ecobank Tanzania, Joyce Ndyetabura akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wanawake pamoja na wajasiriamali waliofika kwenye semina ya mpango maalum ujulikanao kama ‘Ellevate by Ecobank’ iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.