Uchaguzi Malawi unavyoacha somo kwa mataifa ya Afrika

Dar es Salaam. Demokrasia ya Malawi imepiga hatua. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na namna nchi hiyo imekuwa ikisimamia na kuratibu chaguzi zake kwa kuwapa wananchi uhuru na haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka na viongozi kuachiana kijiti bila mivutano.

Tangu taifa hilo limepata uhuru wake mwaka 1964, limekuwa likibadilisha viongozi kupitia chaguzi za kidemokrasia ambapo viongozi wamekuwa wakichaguliwa kwa kuangalia uwezo wao na si vyama wanavyotoka.

Taifa hilo limepata viongozi kutoka vyama tofauti na unapofika wakati wa uchaguzi, wananchi wanapima sera za wagombea na kuamua kuchagua wanaodhani wanafaa kuliongoza taifa lao kwa muhula unaofuata.

Vilevile, Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) imesimama imara katika kutumia uhuru wake kutenda haki. Haijaruhusu wanasiasa hasa kutoka chama kinachokuwa madarakani kuingilia uhuru wao kwa kuwapa maelekezo wala kuingilia Tume ya Uchaguzi.

Jambo hilo limekuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa mengi ya Afrika ambayo mengi yamekuwa na chaguzi za kiini macho, ambazo zinawanyima wananchi haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa njia mbalimbali ikiwemo kukandamiza upinzani.

Pia, Tume za Uchaguzi katika mataifa mengi haziko huru. Zinatekeleza matakwa ya vyama vilivyopo madarakani, jambo ambalo linawanyima haki wananchi na kusababisha vurugu zinazosababishwa na hila hizo.

Katika uchaguzi wa Septemba 16, 2025, MEC imemtangaza Peter Mutharika kutoka DPP kuwa mshindi na hivyo kuwa Rais wa saba wa Malawi, ukiwa ni muhula wake wa pili kwa vipindi tofauti.

Historia ya chaguzi Malawi

Malawi ilipata uhuru wake kupitia chama cha ukombozi cha Malawi Congress Party (MCP) chini ya uongozi wa Hastings Kamuzu Banda. Banda aliliongoza taifa hilo kwa karibu miaka 28 hadi Mei 1994.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1994, mgombea wa chama cha United Democratic Front (UDF), Bakili Muluzi alishinda uchaguzi huo, alimshinda Banda ambaye ndiyo Baba wa Taifa hilo na Rais pekee ambaye Malawi ilikuwa naye tangu uhuru.

Baada ya kumaliza vipindi vyake viwili vya miaka 10 kwa mujibu wa Katiba ya Malawi, Muluzi alistaafu na chama chake cha UDF kikamteua Bingu wa Mutharika kupeperusha bendera kwenye uchaguzi wa Rais wa mwaka 2004.

Mutharika alifanikiwa kushinda uchaguzi huo na kuwa Rais wa tatu wa Malawi. Hata hivyo, aliingia kwenye mgogoro na chama chake cha UDF kilichokuwa kinaongozwa na mtangulizi wake, hivyo mwaka 2005, akaanzisha chama chake cha Democratic Progressive Party (DPP).

Kwa bahati mbaya, Mutharika alifariki dunia Aprili 5, 2012 kutokana na maradhi ya moyo. Kiongozi huyo alifariki katika awamu yake ya pili ya uongozi, akiwa ametumikia urais kwa karibu miaka minane.

Baada ya kifo hicho, aliyekuwa Makamu wa Rais, Joyce Banda aliapishwa kuwa Rais wa Malawi, akiwa Rais wa kwanza mwanamke katika taifa hilo na mmoja wa wanawake wachache barani Afrika kuwahi kuhudumu katika nafasi hiyo.

Ulipofika wakati wa uchaguzi chama chake kikataka kumweka kando ili agombee mdogo wake na marehemu Bingu wa Mutharika, Peter Muthalika lakini akakataa.

Joyce Banda alianzisha chama chake cha People’s Party (PP) baada ya kutimuliwa katika chama cha DPP kwa sababu ya alikataa kumkubali Peter Mutharika kuwa mgombea urais wa DPP kwenye uchaguzi mkuu wa 2014.

Mwanamke huyo alitumikia kama Rais kwa miaka miwili pekee akikamilisha muhula wa Bingu wa Mutharika hadi uchaguzi mkuu wa 2014. Katika uchaguzi huo, Joyce Banda aligombea pamoja na Peter Mutharika na wagombea kutoka vyama vingine bila mafanikio.

Mutharika aliibuka mshindi hivyo akawa Rais wa tano wa Malawi, akimwondoa Banda ofisini. Mutharika aliongoza kipindi cha kwanza kwa miaka sita kutokana na sintofahamu iliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa 2019 kabla ya uchaguzi kurudiwa.

Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Juni 2020, mgombea wa chama cha MCP, Lazarus Chakwera aliibuka mshindi katika uchaguzi huo uliokuwa na msisimko mkubwa na Wamalawi walijawa matumaini na mwanasiasa huyo wa upinzani ambaye pia alikuwa ni kiongozi wa dini.

Hata hivyo, matumaini hayo ya wananchi yalianza kufifia kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi ya utawala wa Chakwera ambaye alituhumiwa kupendelea ndugu zake serikalini huku akifanya ziara za anasa kwa fedha za walipakodi.

Kutokana na hali hiyo katika uchaguzi wa Septemba 16, 2025, Chakwera amepata ushindani mkali kutoka kwa Mutharika aliyeamua kurejea kupambana naye.

Septemba 25, 2025, Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) ilimtangaza Mutharika kuwa mshindi katika uchaguzi huo, akirejea madarakani kwa kipindi chake cha pili.

Katika uchaguzi wa hivi karibuni, MEC imemtangaza rasmi Mutharika kuwa Rais mteule, hivyo kuhitimisha moja ya chaguzi zilizofuatiliwa kwa karibu zaidi katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo.

Akitoa tangazo hilo mjini Lilongwe, Mwenyekiti wa MEC, Jaji Annabel Mtalimanja aliwaeleza Wamalawi safari yote ya uchaguzi, kuanzia uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura, uhakiki wa kura, malalamiko, hadi matokeo ya mwisho; kabla ya kumtangaza Mutharika kuwa mshindi kwa kura 3,035,249, sawa na asilimia 56.8 ya kura halali zilizopigwa.

Hatua mbalimbali za uchaguzo huo zilifanyika kama ambavyo hufanyika katika nchi nyingi, kilicho tofauti na jinsi MEC inavyofanikisha uchaguzi na marais kubadilishana madaraka bila malalamiko.

Kipindi cha uteuzi wa wagombea kilifunguliwa Juni 10 na kufungwa Julai 30, 2025. MEC ilipokea fomu 23 za uteuzi baada ya wagombea kulipa ada ya lazima isiyorejeshwa ya Kwacha 10 milioni (sawa na Sh14 milioni).

Wagombea watatu walijiondoa na 20 waliwasilisha fomu kwa mafanikio. Baada ya uhakiki, wagombea 17 waliteuliwa na walifanya kampeni kuanzia Julai 14 hadi Septemba 14 saa 12 asubuhi.

Jaji Mtalimanja alivipongeza vyama na wagombea kwa kampeni za amani kwa kiasi kikubwa, akisisitiza kuwa walizingatia maadili ya uchaguzi.

Malawi ilikuwa na wapiga kura waliosajiliwa 7,203,390 (wanaume 3,088,670 na wanawake 4,114,720). Kati ya hao, 5,502,982 walipiga kura, sawa na asilimia 76.4 ya ushiriki.

Jumla ya wapiga kura 4,690,314 (asilimia 65.1) walitumia kifaa cha Kielektroniki cha Uhakiki na Utambulisho wa Mpigakura (BVVID).

Katika vituo vingine vya kupigia kura, usajili kwa mikono ulitumika, hali iliyochangia idadi ya juu ya jumla ya wapigakura ikilinganishwa na wale waliotumia mfumo wa kielektroniki.

Jaji Mtalimanja aliwapongeza Wamalawi kwa “uvumilifu wa kusubiri matokeo,” akisisitiza kuwa uchaguzi “huweka ajenda ya kidemokrasia na uongozi wa taifa, na lazima uaminike na umma.”

Akizungumzia uchaguzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema mataifa ya Afrika yana mengi ya kujifunza kwa Malawi ikiwemo kuandaa mazingira ya kisiasa ili kufanya uchaguzi uwe huru na wa haki.

Amesema mazingira ya kisiasa yanahusisha sheria, kanuni na shughuli za kisiasa kwa ujumla, hivyo Malawi imejitahidi kutengeneza mazingira rafiki, ndiyo maana wameweza kufanya uchaguzi wa namna hiyo kwa mara nyingine.

“Jambo jingine tunalojifunza, kwenye nchi nyingi za Kiafrika, siyo rahisi kwa Serikali zilizopo madarakani kuruhusu uchaguzi huru kwa sababu ya matokeo kama ya Malawi. Hapa itategemea uelewa wa watu kushinikiza mabadiliko,” anasema Dk Loisulie.

Kuhusu nafasi ya Tume ya Uchaguzi, mwanazuoni huyo anasema nayo inahitaji kutengenezewa mazingira kwa kuwa inafuata sheria, hivyo ni muhimu kutengeneza sheria na miongozo itakayoifanya Tume kuwa huru kufanya kazi zake kikamilifu bila kuingiliwa.