Folz kuwashushia mziki Waangola Kwa Mkapa

KOCHA wa Yanga, Romain Folz amesema kikosi kipo tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Wiliete akidai  atawashushia mziki kamili Waangola katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Kwa Mkapa, kesho.

Akizungumza leo, Folz amesema hana presha na lolote juu ya kikosi chake kwa kuwa kipo njia salama na kwamba timu  imeshinda mechi zote.

Amesema kutokana na ratiba ngumu ya mechi kuwa karibu mabadiliko ya timu yataendelea ili kuwajenga wachezaji.

Kocha huyo amethibitisha kwamba mchezo wa kesho atashusha kikosi kamili kitakachokwenda kutafuta ushindi licha ya kushinda mechi ya kwanza.

“Matokeo ya mchezo wa kwanza tumeshayaweka kando.  Nimewaambia wachezaji hii ni mechi tofauti na mpya tunatakiwa kutafuta ushindi mwingine ili tufuzu,” amesema Folz.

“Kuhusu mabadiliko ya kikosi yataendelea. Narudia kwa hizi mechi zilizo karibu njia salama ni kuwapa nafasi wachezaji na kuwapumzisha wengine. Kila mchezaji aliye hapa (Yanga) ana kipaji kikubwa.

“Njia salama ni kuwapa nafasi ili waonyeshe (uwezo). Inawezekana baadhi yao kukatokea makosa hatua nzuri ni kujisahihisha.

“Kesho tutakuwa na timu kamili. Tutakuwa na mabadiliko. Tutakuwa na kikosi ambacho kitakwenda kuendeleza kasi yetu ya ushindi.”