Ferry: Hatuna cha kupoteza kesho

Kocha wa Wiliete ya Angola, Bruno Ferry amesema timu yake haina cha kupoteza kwenye mchezo wa kesho ambapo  wataingia na akili ya kubadilisha matokeo.

Ferry amesema wanatambua matokeo mabaya waliyoyapata nyumbani kwao ambayo yalitokana na uchanga wa kikosi  kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wamejipanga kusahihisha makosa.

“Baada ya mchezo wa kwanza tuligundua makosa yetu ambayo tuliyafanya. Tulikuwa na dosari kuzuia tukaruhusu mabao matatu, lakini pia tulifanya makosa kwenye umaliziaji hatukufunga bao lolote,” amesema.

“Tumeyafanyia kazi haya yote. Ukiangalia kiukweli tunakwenda kukutana na wapinzani wenye uzoefu. Wiliete ni timu changa kwenye mashindano kama haya, lakini hatuna cha kupoteza. Kesho tutakwenda kujaribu kuonyesha kitu tofauti.”

Ferry ambaye ni kocha wa zamani wa Azam FC, amesema anajua Yanga itakuwa nyumbani na ina nguvu kubwa mbele ya mashabiki, lakini wachezaji wake watazingatia kile ambacho amewapa ili washinde.

“Naijua Yanga inapokuwa nyumbani sio timu rahisi kukubali kupoteza, lakini natarajia wachezaji wangu watazingatia mambo ambayo nimewaelekeza,” amesema.

Yanga itahitaji sare yoyote au ushindi ili kufuzu hatua inayofuata ya mtoano ikiingia uwanjani na ushindi wa mabao 3-0 ilioupata katika mchezo wa awali uliochezwa jijini Luanda, Angola, wiki iliyopita.