Dodoma. Jumla ya rufaa na malalamiko 108 yanatarajiwa kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Tume ya Utumishi wa Umma kwa muda wa siku 19 kuanzia Septemba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso amesema tume itakutana kujadili rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na waajiri, mamlaka za ajira na za nidhamu.
Mbisso amesema huo utakuwa mkutano wa kwanza wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambao umepangwa kuanza Septemba 29 hadi Oktoba 17, 2025 katika jengo la ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika Mtaa wa Njedengwa, jijini Dodoma.
“Katika mkutano huu, tume inajadili na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka zao za nidahmu. Tunaamini haki itatendeka pasipo shaka,” amesema.
Kifungu cha 12(1)(d) na kifungu 27(1)(b) cha Sheria ya ya Utumishi wa Umma sura 298, tume ina jukumu la kupokea na kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na waajiri wao.
Amesema tume itatoa nafasi kwa warufani na warufaniwa walioomba kufika mbele yake kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa kwani kifungu cha 62(1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 kinatoa nafasi hiyo.
Katika kikao hicho, tume pia itapokea taarifa za utekelezaji wa majukumu katika kipindi cha robo ya tatu na nne kwa mwaka wa fedha 2024/25. Taarifa hiyo itajadiliwa na kutolewa maelekezo mbele ya mkutano.
Mmoja wa waliowahi kufika mbele ya tume ambaye hakutaka kutajwa jina amesema usikilizwaji mbele ya tume una maana kubwa na kwamba, mbali ya kusikiliza, hutolewa ushauri wa wapi mtumishi alikosea na nini akafanye.
“Mimi ni mwalimu, aliyekupa mawasiliano yangu hajakosea ila sipendi kutajwa jina, miaka minne iliyopita nilifukuzwa kazi na mwajiri wangu na ilikuwa ni maonezi, namshukuru Mungu nilipoelekezwa tume waliniita na kunisikiliza hatimaye nilirudishwa kazini na baada ya miezi minne nikalipwa stahiki zangu,” amesema.
Hata hivyo, tume hiyo siyo mamlaka ya mwisho kwani inaelekeza kwa mtumishi ambaye hataridhika anaweza kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutafuta haki zaidi na akiona bado kuna haja, mtumishi huo anaweza kwenda katika vyombo vya sheria ili kutafuta tafsiri ya sheria juu ya uamuzi huo.