Tanzania yasisitiza utatuzi wa migogoro duniani

New York. Tanzania imelaani kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa, hali inayochochea matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro.

Imeeleza kuwa mwenendo huo si tu unadhoofisha juhudi za kimataifa za kudumisha amani na usalama, bali pia unahatarisha maisha ya raia wasio na hatia katika maeneo ya migogoro.

Pia, imesisitiza kuwa matumizi ya nguvu yamekuwa chanzo cha ukatili dhidi ya binadamu, hususan kwa watoto, wanawake, wazee, pamoja na wagonjwa.


Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati akihutubia mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.

Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ametaja udhoofishaji huo ni uwepo wa mitazamo ya kibeberu, ikiwa ni pamoja na ile ya kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya uchukuaji rasilimali na uporaji wa ardhi.

Amesema mitazamo mingine ni kampuni za kimataifa kuendelea kufanikiwa kutokana na unyonyaji wa maliasili za Afrika, huku wakisababisha au kuunga mkono migogoro, hali ambayo inapaswa kumalizika sasa.


Mpango amesema Tanzania inauchukulia msimamo wa upande mmoja na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi, pamoja na kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani kukomesha umwagaji damu na vita vinavyoendelea katika maeneo mengi duniani, ni jambo lisilokubalika.

Pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa ongezeko la matumizi ya fedha katika masuala ya kijeshi ikiwemo utafiti na utengenezaji wa silaha ni jambo la kusikitisha na ni kinyume cha maadili.

Amesema hali hiyo inazuia jitihada za kutafuta amani duniani, na inachukua kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo zingeweza kutumika kuendeleza maendeleo endelevu na ustawi kwa wanadamu wote.

Kwa mujibu wa Mpango, dunia inapaswa kuendelea kutafuta amani bila kuchoka kwani ndio sharti la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo, amepongeza juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres na viongozi wengine wa dunia kwa kuendeleza juhudi za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro kama vile Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Russia, Ukraine na Mashariki ya Kati.

Ametoa wito wa ushirikishwaji kamili wa wanawake katika kutafuta amani hususani katika kipindi hiki inaposherehekewa miaka 30 tangu azimio la Beijing na  maendeleo yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Amesema Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia katika kueleza sera na vitendo vinavyoimarisha nafasi ya mwanamke katika sekta zote za jamii.

Mpango amesema kikanda na kimataifa, amekuwa mtetezi wa amani, haki, usalama na matumizi ya nishati safi.

Pia, amesema Tanzania imetangaza kugombea kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2029-2030, ili kuthibitisha dhamira iliyonayo ya amani na usalama duniani.

Mpango pia, amesema Tanzania inasisitiza msimamo wa Afrika wa kurekebisha uwakilishi mdogo wa bara hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kutoa wito wa kupitishwa kwa angalau viti viwili vya kudumu vya Afrika, vyenye nguvu ya kura ya turufu.