Mke alia mumewe kutoweka katika mazingira tata

Moshi. “Ninamuombea msamaha mume wangu kwa watu wanaomshikilia, naombeni mnisamehe na mimi kama mke wake na muwasamehe watoto niliozaa naye kwa sababu adhabu mnayompa Joseph hata mimi inanipata, tena inanipata zaidi kuliko huyo mnayemshikilia kwa sababu sijui alipo, kwa nini mnatutesa hivi?”

Ni kauli ya Rehema Seleman (27), mkazi wa Kata ya Ng’ambo, mjini Moshi akielezea mateso anayopitia yeye na watoto wake wawili kutokana na mume wake, Joseph Lema (28), kutoweka katika mazingira yenye utata.

Akizungumza na Mwananchi jana Septemba 25, amesema watu wasiojulikana walimpigia simu mume wake Julai 22, 2025 wakimwitia kazi na tangu siku hiyo hajawahi kuonekana.

Rehema amewaomba watu wanaomshikilia mumewe wampe adhabu kama anakosa, ili yeye na watoto wapate fursa ya kumtembelea alipo, kuliko maumivu ya kiakili na kisaikilojia wanayoyapitia.

Rehema, mama wa watoto wa kiume mwenye miaka minne na wa kike wa miezi mitatu, anadai Julai 22, 2025, mumewe Lema alipigiwa simu na namba isiyojulikana kwa ajili ya kazi, akaondoka kwenda kuonana na wahusika, na tangu siku hiyo hajapatikana.

Picha ya Joseph Shedrack Lema, mkazi wa Kata ya Ng’ambo wilayani Moshi Mkoani kilimanjaro anayedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha  tangu Julai 22, 2025



Amesema siku hiyo mumewe ambaye ni fundi ujenzi aliagizwa afike jirani na Shule ya Sekondari Msaranga kwa ajili ya kazi ya ufundi.

Rehema amesema aliondoka saa tano asubuhi kwa kutumia baiskeli na tangu wakati huo simu yake haikupatikana hewani.

Amesema kutokana na hilo alikwenda kwa mama mkwe wake kuuliza iwapo Lema alikuwa amelala huko, alielezwa hakumuona hali iliyongeza wasiwasi, hivyo alianza ufuatiliaji kwa marafiki na majirani.

Anaeleza alifika shule ya Msaranga ambako baadhi ya wanafunzi walisema waliona baiskeli imeegeshwa ukutani saa 11:00 jioni, lakini baadaye haikuonekana tena.

Rehema amesema baadaye alipata taarifa kuwa gari jeusi aina ya Toyota RAV4 liliingia eneo hilo na kumchukua mumewe, na alionekana akipanda pasipo kusukumwa wala kulazimishwa.

“Walisema walimwona akipanda gari akiwa na watu waliokuwa na nywele za rasta, kisha gari likaondoka na baiskeli akabaki pale,” amesema.

Anaeleza baiskeli hiyo, ambayo awali ilionekana ikichezewa na watoto wa shule, baadaye iliokotwa na mtu aliyekuwa akipita eneo hilo na kupelekwa ofisi ya mtaa, kabla ya kuchukuliwa na baba wa Lema kwa ajili ya kuihifadhi.

Rehema amesema alikwenda kufungua jalada la kutoweka kwa mumewe katika Kituo cha Polisi Majengo na baadaye kufikisha taarifa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi.

Hata hivyo, anasema hadi sasa hajapatiwa majibu ya uchunguzi, zaidi ya kuambiwa Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia.

Rehema amesema kupotea kwa mumewe kumemsababishia matatizo makubwa ya kisaikolojia na kifamilia.

“Niliishi wiki nzima bila kula. Siyo kwamba chakula hakipo, bali hamu ya kula haipo. Hali hii iliathiri hata afya ya mtoto wangu mdogo,” amesema.

Amesema mtoto wao wa miaka minne humuuliza mara kwa mara kuhusu baba yake hali inayomuumiza zaidi.

“Juzi aliniuliza mama, mbona baba haji? Maswali hayo huniumiza sana kwa sababu sina jibu la uhakika,” amesema.

Kwa sasa, Rehema anasema anategemea msaada wa shemeji yake Joshua Lema na wakwe zake ambao wamekuwa wakimhudumia, huku marafiki wa mumewe wakijitolea kumjengea banda dogo la biashara nyumbani kwake na kuahidi kumpatia mtaji ili aweze kujikimu kimaisha na watoto wake.

Joshua Shedrack, mdogo wake Lema, amesema siku ya tukio walikuwa wote nyumbani hadi mchana alipopigiwa simu na mtu aliyemwita afike jirani na Shule ya Msaranga.

“Kesho yake tulipojaribu kumpigia hakuonekana wala kupatikana. Tulienda polisi na kuzunguka magereza ya Arusha na Moshi bila kupata taarifa zozote,” amesema.

Amesema familia kwa sasa imeamua kumwachia Mungu suala hilo baada ya jitihada zao zote kushindikana. “Wanayemshikilia tunaomba waonyeshe utu, waturudishie ndugu yetu. Tumekubaliana kama familia kwamba tumwachie Mungu atende muujiza,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 26, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema jeshi hilo linazo taarifa za kupotea kwa mtu huyo na uchunguzi wa kisayansi kujua alipo unaendelea.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mnazi katani humo, Mary Joseph amesema tukio la kutoweka kwa mwananchi huyo linawaacha na maswali mengi kwa kuwa tangu taarifa ilipotolewa hajaonekana.