Moshi. Mgombea udiwani wa Kata ya Marangu Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Innocent Shirima ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, barabara za ndani pamoja na ajira kwa vijana.
Akizungumza leo Septemba 26, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Marangu Mtoni, Shirima amesema changamoto kubwa kwa wananchi wa kata hiyo ni tatizo la maji, licha ya eneo hilo kuwa na vyanzo vingi vya maji.
“Marangu Mashariki ndiyo tunalinda vyanzo vya maji, lakini jambo la kusikitisha wananchi bado wanateseka kupata maji. Nipeni nafasi, nitapambana kuhakikisha tunapata maji ya uhakika kwa kina mama na wananchi wote,” amesema Shirima.
Ameongeza kuwa, endapo atachaguliwa, yeye pamoja na mgombea ubunge kupitia chama hicho, Enock Koola watahakikisha barabara za ndani za kata hiyo zinapitika kwa msimu wote.
“Nipeni nafasi tupambane tupate hata fungu dogo la kuanza kufungua barabara zetu. Nitaungana na Koola kupata vifaa na kushirikisha wananchi ili tuweze kuzifungua wenyewe,” amesisitiza.
Kuhusu ajira, Shirima amesema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira hali inayowasukuma kujiingiza kwenye ulevi, licha ya Mlima Kilimanjaro kuwa fursa kubwa ya mapato kupitia utalii.
“Nitahakikisha biashara ya utalii katika Mlima Kilimanjaro inanufaisha vijana wetu na kufungua fursa za ajira. Pia, ndoto yangu ni kuhakikisha ndani ya miaka mitano hakuna mtoto atakayeshindwa kwenda kidato cha kwanza kwa sababu ya kukosa vifaa vya shule au sare,” amesema.
Akizungumzia mazingira ya biashara katika soko la Marangu Mtoni, Shirima ameahidi kujenga vyoo vya kisasa vyenye matundu 10 hadi 16 ili wafanyabiashara wafanye biashara katika mazingira salama na yenye staha.
Aidha, amesema atashirikiana na Koola katika kusaidia vijana, kina mama na watu wenye ulemavu kuandika maandiko bora ya miradi ili waweze kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Vunjo, Enock Koola amesema endapo wananchi wa kata hiyo watamchagua pamoja na Shirima watashirikiana kuweka mikakati madhubuti ya kupambana na tatizo la maji katika kata hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitano.
“Ukanda wetu wa juu tuna shida sana ya maji, tupeni kura za kishindo ili miaka mitano ijayo tupambane tumalize kero ya maji, ibaki kuwa historia”amesema Koola
Kuhusu suala la barabara za ndani za kata hiyo, amesema atahakikisha analeta mitambo maalumu ya kuchimba barabara hizo ili ziweze kupitika wakati wote na wananchi waweze kufanya shughuli zao za usafirishaji bila changamoto.
Amesema tayari wameshaanza kutengeneza baadhi ya barabara za kata ya Mwika kusini, ambapo wana mitambo ya greda, Eskaveta na roller na wanasubiri muda ufike wayapeleke Marangu Mashariki.
“Tunachoomba ndugu zangu ni kura za Rais Samia Suluhu Hassan ili tupate haya maendeleo tunayozungumza ya mitambo ili matatizo yetu yaweze kutatuliwa, mkitupa ridhaa tutaweka mikakati mizuri ya kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wetu.”amesema Koola
Ameongeza “Katika kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan miradi mingi ya maendeleo imefanikishwa, ikiwemo sekta za afya na elimu. Shukrani kubwa kwa Rais Samia ni kuhakikisha tunampatia kura nyingi pamoja na wabunge na madiwani wa CCM ili miradi ya maendeleo iendelee kwa kasi,”