NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
WANAFUNZI wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wamebuni vifaa maalum vya elimu ya vitendo vinavyojulikana kama Train Kits, vilivyotengenezwa hapa Tanzania kwa kutumia rasilimali za ndani.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Kitaifa yanayoendelea Ukumbi wa Mlimani City, Hosea Kimaro, mwanafunzi wa DIT na Mkurugenzi Mtendaji wa Honic Company Limited, amesema kuwa Train Kits zimetengenezwa kusaidia shule na taasisi mbalimbali kutatua changamoto ya upungufu wa vifaa vya majaribio, changamoto iliyokuwa ikizuia wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi na teknolojia kwa vitendo.
“Vifaa hivi ni nafuu na vinaweza kupatikana kwa urahisi na shule nyingi. Lengo letu ni kuziba pengo lililopo kati ya elimu ya nadharia na ile ya vitendo,” amesema Hosea.
Amesema kuwa vifaa hivi vitasaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na fani nyingine zinazohitaji mafunzo ya vitendo.
Aidha, mradi huo unalingana na sera ya sasa ya elimu nchini, inayolenga kutoa elimu ya amali, ambapo wanafunzi wanapata ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja kazini au katika maisha halisi.
Hosea ameongeza kuwa kupitia Honic Train Kits, kampuni yake inachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa dira ya elimu ya Tanzania, ikihakikisha kuwa wanafunzi wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.