Wananchi wahamasishwa kutumia fursa ya ujio wa Mwenge Rukwa

Rukwa. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamesema ujio wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni fursa ya kiuchumi hususan kwa wafanyabiashara wadogo na sekta ya usafirishaji.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 26, 2025, baadhi ya wafanyabiashara wa vyakula na watoa huduma za usafiri, wamesema Mwenge wa Uhuru utaongeza mzunguko wa fedha na kuongeza kipato chao kutokana na wingi wa watu watakaoshiriki katika mbio hizo.

“Ni fursa kwetu, mwenge wa uhuru utakesha hapa manispaa ya Sumbawanga wananchi watakula na kunywa kwa hivyo tutafanya biashara ya chakula na kujifunza fursa nyingine kutokana na miradi itakayozinduliwa,” amesema Sophia Katunka.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere amesema Mwenge wa Uhuru utawasili mkoani humo Septemba 28, 2025 katika Kijiji cha Kizi, Kata ya Paramawe, katika mji wa Namanyere, halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Amefafanua kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 653.1 na unatarajiwa kuzindua jumla ya miradi 34 yenye thamani ya Sh55.3 bilioni.

Kati ya miradi hiyo, miradi saba itazinduliwa rasmi, miradi 15 itawekewa mawe ya msingi huku miradi mingine 12 ikitarajiwa kukaguliwa.

“Niwaombe wananchi ushirikiano mnaouonyesha katika mapokezi ya viongozi ndio tuonyeshe katika mapokezi ya mwenge wa uhuru,” amesema Makongoro.

Ofisa Usafirishaji, Anordi Shayo amesema ujio wa mwenge ni fursa kwa vijana kusafirisha abiria hasa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.

Sambamba na hilo, mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kutangaza ujio wa mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan Oktoba 18, 2025 ambapo atazungumza na wananchi na kunadi sera za chama hicho.