Watatu walioshtakiwa kwa mauaji akiwemo mtalaka, waachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Morogoro imewaachia huru watuhumiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kumuua Marietha Petro na kuutelekeza mwili wake kando ya barabara.

Watuhumiwa waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo ni Stanley Winfred, Dabobertus Natalis (ambaye awali alikuwa mume wa Marietha kabla hawajaachana kwa kupeana talaka) pamoja na Magnus Anton.

Wote watatu walikuwa wakishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Mei 13, 2024 katika Kijiji cha Utengule, Kata ya Mlimba mkoani Morogoro.

Hukumu hiyo ya kuwaachia huru washtakiwa ilitolewa Septemba 19, 2025 na Jaji Steven Magoiga, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote na vielelezo vilivyowasilishwa, Jaji Magoiga alisema Mahakama imewaachia huru washtakiwa kutokana upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yao.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba na vielelezo vinne huku utetezi kukiwa na mashahidi watatu (washtakiwa).

Baada ya mshtakiwa wa kwanza (Stanley), kukamatwa alikiri kumuua marehemu kwa maagizo na malipo kutoka kwa mshtakiwa wa pili na tatu.

Shahidi wa kwanza, mtoto wa marehemu aliyekuwa na umri wa miaka 10, alieleza kuwa siku ya tukio, mama yake aliondoka nyumbani na kumwambia alipeleka barua kwa Sadi, akiwa na mshtakiwa wa kwanza.

Alidai kuwa mama yake hakurudi nyumbani na kwamba siku tano baadaye, Mei 18, 2024, maiti ilikutwa msituni ambapo polisi walifanya uchunguzi na daktari alibaini kuwa mwili huo ulikuwa umeoza, na sampuli za DNA zilithibitisha kuwa ulikuwa wa Marietha.

Shahidi huyo alidai kumfahamu mshtakiwa wa pili kwani ni baba yake mzazi ambaye licha ya kuwa alishaachana na mama yake,alikuwa akiwatembelea nyumbani mara kwa mara na kuwa mshtakiwa wa tatu alikuwa baba yake wa kambo na kuhitimisha ushahidi wake kuwa hakuwahi kuona aliyemuua mama yake.

Shahidi mwingine, ASP Lugano Mwakisunga, alieleza kuwa walitembelea eneo la tukio Mei 18, 2024, na kukuta mwili wa marehemu, ambao ndugu walimtambua kupitia mavazi.

Aliongeza kuwa mshtakiwa wa kwanza alikamatwa Juni 5, 2024, na alikiri kumuua Marietha kwa maelekezo ya mshtakiwa wa pili na tatu, na kwamba alipokea Sh 150,000 kati ya Sh 250,000 alizoahidiwa.

Katika utetezi wao, washtakiwa walikanusha tuhuma hizo za mauaji ambapo Stanley alidai kuwa Mei 13, 2024, alikuwa nyumbani kwake na hakwenda nyumbani kwa marehemu kama ilivyodaiwa na shahidi wa upande wa mashtaka.

Alidai kuwa alikamatwa Juni 5, 2024, na kupigwa sana na kulazimishwa kusaini maelezo ya onyo yaliyokuwa yameandikwa na polisi na kuwa alipigwa kiasi cha kushindwa kutembea.

Dabobertus alikiri kwamba marehemu alikuwa mke wake zamani, ila walishaachana na kupeana talaka huku akikanusha kuwa na mgogoro wowote na marehemu, akisema kuwa aliishi umbali wa kilomita 50 kutoka eneo la tukio.

Alidai kuanzia Mei 8, 2024 hadi Mei 18, 2024 alikuwa katika kambi ya wavuvi ya Mtoni Kapemba.

Kwa upande wake, Magnus alikana kuhusika na tukio hilo na kuieleza mahakama kuwa hakuwahi kutoa wala kumpa mshtakiwa wa kwanza kazi yoyote.

Mshtakiwa huyo aliithibitishia mahakama kuwa alikuwa na uhusianao wa kimapenzi na marehemu na kukana madai ya kuwa na mgogoro naye wa ardhi.

Jaji amesema, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo, mahakama itaangalia iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kosa la mauaji kwa kiwango kinachotakiwa katika kesi za jinai.

Amesema ili kuthibitisha hatia ya mauaji dhidi ya washtakiwa, upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha iwapo Marietha alifariki dunia,kifo chake kilikuwa cha kawaida au la na kama washtakiwa ndio waliohusika na mauaji hayo na mwisho ni iwapo yalikuwa ya kukusudia au la.

Jaji Magoiga amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, hakuna ubishani kuwa Marietha alifariki dunai na mwili wake ulikutwa ukiwa umeanza kuoza kando ya barabara ambapo hilo lilithibitishwa na shahidi wa pili, tano na uchambuzi wa DNA.

Kuhusu washtakiwa kuhusika na mauaji hayo, Jaji amesema upande wa mashtaka unategemea vipande viwili vya ushahidi katika suala hilo ambapo shahidi wa kwanza wa Jamhuri alidai mshtakiwa wa kwanza aliondoka na Marietha nyumbani kwake.

Ushahidi mwingine ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza ambapo amenukuliwa akikiri kusababisha mauaji hayo na kuwahusisha washtakiwa wenzake.

Kuhusu maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, Jaji amesema mshtakiwa alikiri kumyonga marehemu hadi kufa na kabla ya hapo alimfanyia udhalilishaji kwa kumbaka.

Jaji amesema mshtakiwa alidai kuteswa kwa kupigwa kiasi cha kushindwa kutembea na kulazimishwa kusaini maelezo hayo ambapo alinukuu mashauri mbalimbali ya mahakama ya rufaa na kuhitimisha kuwa mahakama inaona maelezo hayo yanakabiliwa na udhaifu mkubwa.

“Kwenye kielelezo cha nne ilidaiwa mshtakiwa wa pili n awa tatu walikuwa na mgogoro wa wa shamba na marehemu lakini hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri aliyetoa ushahidi kuhusu madai hayo,”amesema Jaji.

Baada ya uchambuzi wa ushahidi wote na vielelezo,Jaji alihitimisha kuwa hakuna ushahidi wa kuaminika kwenye rekodi wa kuwahusisha washtakiwa na kosa hilo.

Jaji Magoiga alieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa hilo dhidi ya washtakiwa hao na kuamuru waachiliwe huru, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine yoyote.