Polisi yaanza kwa kipigo Zanzibar

UHAMIAJI imejiandikia rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika Ligi Kuu Zanzibar kufunga bao na kupata ushindi ikiwa ugenini huku mchezaji wake akionyeshwa kadi nyekundu.

Mechi iliyofanyika Septemba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, Mjini Unguja, dakika 90 zilimalizika kwa Uhamiaji kutoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi iliyopanda daraja msimu huu.

Mohamed Mussa, amefungua pazia la Ligi kwa kufunga bao la kwanza la msimu dakika ya 32, huku Adam Issa akikumbana na adhabu ya kadi nyekundu.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh amesema timu hiyo kuonyeshwa kadi kwa mechi ya kwanza, bado haijawa athari kwao kwani wana kikosi kipana kinachoweza kuziba nafasi hiyo.

UHA 01


Akizungumzia ushindi huo, amesema katika kipindi cha maandalizi ya ligi alitumia nafasi hiyo kukijenga kikosi chake kimwili, kisaikolojia na kiufundi ndio sababu ya kuanza vizuri.

“Kadi nyekundu haijawa na athari kwetu, tuna kikosi kipana chenye uwezo wa kufanya vizuri katika mechi zijazo,” amesema kocha huyo.

Kocha Mkuu wa Polisi, Nassor Salum alisema licha kupoteza mchezo huo bado ana kikosi bora ambacho kitatoa matokeo mazuri hapo baadaye.

Alisema, mpinzani wake alimzidi katika eneo la kati ambalo ndilo alilolitumia kutengeneza mashambulizi na kuzaa bao kipindi cha kwanza.

UHA 02


Nassor amesema hiyo ilichangia kipindi cha pili kuanza kwa mabadiliko ya kiufundi kwa kumuingiza kiungo Rashid Mohammed  ambaye alileta uhai wa timu eneo la kati lililoonekana kuzidiwa kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, juhudi za mabadiliko hayo hazikuzaa matunda upande wao ambapo dakika 90 zilimalizika kwa Uhamiaji ikiwa inaongoza bao 1-0.