Fundi wa boli Fountain gate ala kiapo

KIUNGO fundi wa mpira wa Fountain Gate, Elie Mokono aliyeisumbua ngome ya Simba jana usiku kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara amekula kiapo akisema anaamini kikosi chao kitarejea katika mwenendo mzuri kama ilivyokuwa mwanzoni mwa  2024/25.

Fountain Gate iliyolazimika kuivaa Simba ikiwa na wachezaji 13 na kupasuka kwa mabao 3-0 awali ilianza msimu kwa kuchapwa 1-0 na Mbeya City.

Mokono ambaye ni raia wa Burundi licha ya kuzaliwa Kinshasa, DR Congo alisema haiwavunji moyo kupoteza wa sababu kikosi kina morali kubwa na kiko kwenye mchakato wa kurekebisha makosa.

“Tulianza msimu vibaya lakini Fountain Gate si timu ya kukata tamaa. Tuna kikosi kizuri na tukiwa kamili naamini tutakuwa tofauti kabisa. Huu ni mwanzo bado ligi ni ndefu na tuna muda wa kurudi kwenye mstari,”  alisema. Nyota huyo ambaye msimu uliopita alifunga mabao saba, aliongeza kuwa, “kwa uchezaji wetu dhidi ya Simba kila mmoja aliona tunaweza kupambana na timu kubwa. Hilo linatupa imani kuwa tukiwa timamu Fountain Gate itakuwa timu tishio.”

Msimu wa  2024/25, Fountain Gate iliongoza msimamo wa ligi kwa muda ikishinda mechi mbili na sare mbili ambao ulikuwa mzuri kwao tofauti na uliopita ambapo walijikuta wakinusurika kushuka daraja.