Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha inayowakabili watu tisa wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi, imeiomba siku 21 kukamilisha upelelezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato ameeleza hayo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Septemba 25, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi PF. 19931 Fredrick Malekela (45) mkazi wa Kilwa Road, E. 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54) mkazi wa Chanika, E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54) mkazi wa Kibamba, F.1126 Sajenti Robert Titus (47) mkazi wa Kisarawe, F.5092 Sajenti John Kaposwe (46) mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi (30) mkazi wa Kisarawe.
Wengine ambao siyo maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59) mkulima na mkazi wa Chanika, Simon Aloyce (60) mfanyabiashara mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29) mfanyabiashara mkazi wa Tataba.
Kato amesema kuna vitu vichache ambavyo wanamalizia na hivyo ameomba mahakama iwapatie muda ili waweze kukamilisha upelelezi huo.
Kato baada ya kutoa ombi hilo, wakili anayemtetea mshtakiwa Malekela na Moshi, George Mwalaki ameiomba mahakama ipange siku 14 badala ya siku 21 zilizoombwa na upande wa mashtaka.
Ombi hilo pia lilipingwa na washtakiwa kwa kuwa wengi wao wanatoka nje ya Dar es Salaam wakidai nauli ni tatizo kwao, hivyo waliomba mahakama itoe muongozo wa kuahirisha kesi hiyo.
“Mheshimiwa hakimu, siku 14 kwangu zitakuwa zinanibana kwa sababu natokea Mwanza, kila baada ya siku 14 nakuja mahakamani, kidogo kwangu siku hizo zitakuwa zinanibana kwa sababu ya nauli,” alidai mshtakiwa Simon Aloyce.
Mshtakiwa mwingine ni WP 10050 Julieth Moshi (30) mkazi wa Kisarawe ambaye naye aliomba mahakama isogeze mbele tarehe za kesi hiyo.
“Mheshimiwa hakimu, siku 14 zinatubana wengi kutokana na kutafuta nauli, hivyo tunaomba isogeze mbele tarehe ya kesi yetu,” aliomba mshtakiwa Julieth.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, alisema kwa kuwa washtakiwa wapo nje kwa dhamana, kesi anaiahirisha hadi Oktoba 23, 2025 itakapotajwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na kesi hiyo ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025, yenye mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo, kinyume na vifungu namba 333, 335A na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Katika mashtaka yao, wanadaiwa kuwa vibali hivyo, vilitolewa kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha cha Desemba 5, 2024 chenye jina la Ahmed Ally, wakijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili hadi la 13, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walitengeneza vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim kinyume cha sheria.
Shtaka la 14 hadi 16, washtakiwa hao wanadaiwa mwaka 2025 katika mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Julai 28, 2025 na kusomewa mashtaka hayo ambayo waliyakana na wapo nje kwa dhamana.