Dodoma. Wakati msichana mmoja kati ya wanne akipata mimba kati ya miaka 15-19, wataalamu wa afya wamesema ukimya wa wazazi, jamii na malezi yasiyofaa ndio chanzo cha wengi kuingia katika janga hilo.
Wameeleza kuwa kutokujua ni lini mzazi aanze kuzungumza na kijana wake wa kike, kiume kuhusu afya ya uzazi huchangia mtoto kupata elimu isiyofaa kutoka kwa watu wasiofaa, hivyo kujikuta wakipata mimba za mapema.
Hayo yamezungumzwa Alhamisi, Septemba 25, 2025 na msimamizi wa maendeleo ya biashara kutoka Shirika la Marie Stopes, Dk Mashingo Lerise mara baada ya kutoa elimu kwa vijana hao kutoka shule mbalimbali za sekondari jijini Dodoma.
“Vijana ndiyo sehemu muhimu kwa nchi yetu na takwimu za TDHS zinaonyesha mpaka mwaka 2022 binti mmoja kati ya wanne amepata ujauzito akiwa na umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 na hii inadhihirika wazi kwamba wengi hawana elimu sahihi,” amesema.
Amesema baadhi ya vijana waliokutana nao wanaonekana wana taarifa ambazo si sahihi, kwani wengi waliuliza maswali yakionyesha wazi wanatamani kufahamu zaidi kuhusu afya ya uzazi, hivyo imewaweka katika nafasi nzuri kama wataalamu, kufahamu nini vijana hao wanahitaji.
Amesema kwenye makundi waliyokutana nayo, wengi wana shauku kuuliza kuhusu njia za uzazi wa mpango na wengine wanataka kujua kondomu zikoje, wanafundishwa lakini hawajawahi kuona picha, hapa wanajifunza na tunaelekeza vijana namna ya kujilinda, wengi wana maswali ambayo wanajijibu wenyewe, elimu bado inahitajika kwa kundi hili.”
Amesema vijana wengi wana elimu kuhusu kuangalia picha au nyimbo ambazo zinaweza kuwaweka kwenye vishawishi.

Mkufunzi wa elimu ya afya ya uzazi, Mgeni Kisesa akizungumza na vijana mbalimbali jinsi ya kujikinga na vishawishi vinavyoweza kuwaletea athari ikiwemo mimba na magonjwa mbalimbali yatokanayo na ngono isiyo salama.
“Tumewafikia wengi, jana (Alhamisi) tulifanikiwa kuwafikia vijana 500, leo tunao 500 na kesho tutakuwa na vijana 500, wataondoka na hii taarifa, hivyo tunaamini wataweza kuwapa taarifa hii wengi zaidi,” amesema.
Pamoja na hayo, amesema hatari kubwa kwa kundi hilo ipo kwenye mitandao ya kijamii kwani maudhui mengi yamekuwa yakipotosha taarifa nyingi kuhusu afya ya uzazi na kuwataka vijana wawe makini na taarifa hizo.
Ametahadharisha kuwa ni muhimu kutafuta taarifa sahihi na ikiwezekana kupiga hata namba za simu kupata usaidizi wa taarifa na nyakati zingine watembelee kurasa sahihi zikiwemo za Wizara ya Afya au Marie Stopes.
Amesema wazazi wana jukumu kubwa kwani si kazi rahisi kuzungumza na kijana ukiangalia mila zetu na desturi; ni suala ambalo halizungumzwi kwa uwazi na vijana wanataka kupata taarifa.
Hata hivyo, anategua kitendawili cha lini mzazi anatakiwa kusema na mtoto wake.
“Kwa mzazi, pale mwanao anapoanza kukuuliza maswali kuhusu afya ya uzazi anza naye. Tukisema miaka 13 huenda ukawa umechelewa; ule ndiyo wakati sahihi kutafuta lugha rahisi. Ukimdanganya kwa kudhani kwamba kuficha ukweli unamwokoa, siku akipata taarifa sahihi atahisi hujui, au unajua ila muongo, na akikuona muongo hatakuamini katika mengine,” amesema.
Amesisitiza kuwa muhimu taarifa sahihi aipate kwa mtu sahihi kabla hajakutana na mtu asiye sahihi akamfundisha tofauti.
Miongoni mwa elimu ambayo wameipata vijana hao ni pamoja na afya, uzazi wa mpango pamoja na kuzuia na kutibu.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisasa waliozungumza na Mwananchi wamesema walikosa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi na wamenufaika kupata elimu hiyo.
“Kuna vitu vingi hatukuvijua, tumefanikiwa kujifunza leo na tunaamini hata wazazi wasingetupa elimu hii. Binafsi imenisaidia kama msichana, sasa najua nitafuata ndoto zangu,” amesema mwanafunzi mmoja.
Mtaalamu wa masuala ya masoko, Marie Stopes, Erick Asenga amesema vijana hao wamejifunza mambo kadhaa pia kuhusiana na bidhaa za afya mbalimbali za uzazi wa mpango.