Abbas Mwinyi azikwa Mangapwani, vigogo wahudhuria mazishi

Unguja. Wakati aliyekuwa mgombea ubunge wa Fuoni, Abbas Mwinyi akizikwa, baadhi ya wananchi kisiwani hapa wamemweleza namna ambavyo alikuwa mpole na hakupenda makuu.

Abbas ambaye ni kaka wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana, Septemba 25, 2025 katika Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi Lumumba alipokuwa akipatiwa matibabu na amezikwa leo Septemba 26, 2025 katika makaburi ya familia huko Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Swala ya jeneza imeongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab katika msikiti wa Zinjibar na swala ya mwili wa marehemu Mangapwani imeongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir.


Abbas ambaye licha ya kuwa mtoto wa Rais wa tatu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi, hakuwa maarufu hata baada ya kuingia kwenye siasa alipostaafu kazi zake za urubani.

Aliingia kwenye siasa mwaka 2020 ambapo alichaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo alikuwa pia mgombea wa nafasi hiyo katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaofanyika Oktoba 2025.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amepokea mkono wa pole kufuatia kifo cha kaka yake, Abbas Ali Mwinyi, kilichotokea jana Septemba 25, 2025.

Katika kuonesha mshikamano wa kitaifa kwa familia ya marehemu Abbas Mwinyi, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, walifika kutoa mkono wa pole nyumbani kwa familia Bweleo, Mkoa wa Mjini Magharibi B.



Kutokana na kifo chake, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeahirisha uchaguzi katika jimbo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, mwanasiasa mkongwe na mkazi wa Fuoni, Ali Makame amesema Abbas hakuwa maarufu sio tu bungeni, hata jimboni mwake, lakini alikuwa makini katika utendaji wake.


“Hakika ni pigo kuondokewa na mpendwa wetu, mimi pamoja na kuwa kwenye siasa lakini bwana Abbas hakuwa mtu wa siasa kwa kweli, hata alipostaafu kazi yake na kuingia kwenye siasa, sio mtu ambaye ungemwona sana katika majukwaa ya kisiasa,” amesema.

“Inawezekana hata alikuwa hajulikani licha ya umaarufu wa baba yao na kaka yake,” amesema Makame.


Kutokana na kifo cha Abbas, shughuli za kampeni ambazo zilikuwa zinaendelea sio tu za mdogo wake, Dk Mwinyi, aliyekuwa ziarani Pemba, bali hata ACT Wazalendo walisitisha mikutano yao iliyokuwa ifanyike katika eneo la Mangapwani alipozikwa katika makaburi ya familia.

Wakati kifo kinatokea Septemba 25, 2025, Dk Mwinyi alikuwa Pemba ambapo alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumkabidhi mkandarasi ujenzi wa miradi miwili ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba na barabara yenye urefu wa kilometa 43.5 kutoka Chakechake hadi Mkoani.


Ilimlazimu Dk Mwinyi aondoke na shughuli hiyo alimwagiza Makamu wa Pili, Hemed Suleiman Abdulla kumwakilisha. Pia, Dk Mwinyi ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Septemba 27, 2027 alikuwa awakabidhi hati za mashamba ya karafuu wakulima kisiwani Pemba.

Vigogo wahudhuria mazishi

Katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa kwa familia ya mzee Mwinyi, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wamefika kutoa mkono wa pole nyumbani kwa familia Bweleo, Mkoa wa Mjini Magharibi B.


Miongoni mwa walioungana na Rais Samia ni Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dk Tulia Ackson, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Hemed Suleiman Abdulla.

Wengine ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuberi Ali Maulid, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro, mgombea mwenza wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.