DK.SAMIA:SERIKALI IMESHATUMIA BILIONI 726/- KWA AJILI PEMBEJEO KWA WAKULIMA

Na  Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali imeshatumia Sh.bilioni  726 kwa ajili ya kugawa pembejeo za ruzuku kote nchini.

Amesema kuanzia mwaka 2021/22 Serikali ilifanya maamuzi kuanza mfumo wa ruzuku za pembejeo katika zao la korosho na mpaka sasa pembejeo zimekuwa zikitolewa bure huku kiwango kikiongezeka kila mwaka.

Akizungumza leo Septemba 26,2025 alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara alipokuwa akihitimisha mikutano yake ya kampeni kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka 2025.

“Natunatumia Sh.bilioni 192 kila mwaka fedha ambayo ingekuwa inatoka mfukoni kwa wakulima lakini tumezibakisha mifukoni kwao, serikali tunagawa kwa ruzuku.

Alisisitiza: “Mbolea, salfa, dawa za kuua wadudu bure Serikali inatoa bure. Kwa hiyo ndugu zangu Serikali inafanya hivyo kwa sababu tumedhamiria kukuza kilimo, uzalishaji wa korosho.”

Akieleza zaidi Dk. Samia amesema uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 118,000 mwaka 2021 ambazo zilikuwa na thamani ya sh. bilioni 265 hadi kufikia tani 330,505 zilizouzwa msimu uliopita zikiwa na thamani ya sh. trilioni 1.9 ambazo zimeingia kwa wakulima.

Amesema kuwa hayo ni manufaa makubwa kwa wakulima kwani bila ruzuku uzalishaji ungeshuka na mapato kwa wakulima yangeshuka.

Pia ameahidi  serikali itaendelea kutoa huduma hizo kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji.

“Nchi yetu ni ya pili kwa Afrika katika uzalishaji korosho, wanaotupita ni Ivory Coast lakini wa pili ni sisi. Tutaendelea kuweka jitihada ili twende sambamba na nchi hiyo ambayo sasa inaongoza.

“Jitihada hizi zimechangia kuongeza uzalishaji siyo tu katika korosho bali pia kwenye mbaazi na ufuta. Uwekezaji mwingine ni kuongezeka kwa skimu za umwagiliaji.”

Pia Dk.Samia amesema  skimu hizo katika mkoa huo zipatazo 66, kuna miradi miwili mikubwa yenye thamani ya sh. bilioni 38.6 inayojengwa Ndanda (Masasi) na Arusha chini (Newala).

Amesema endapo CCM ikipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, itaendelea kutafuta masoko yenye uhakika siyo tu kwa zao la korosho bali mazao yote.

Mgombea Dk.Samia amesema serikali itaendelea kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa kongani ya viwanda iliyopo kijiji cha Maranje wilayani Mtwara.

Pia, alisema serikali itaendelea kusimamia kwa karibu vyama vya ushirika ili kuondoa ubadhirifu wa fedha za wanaushirika lakini pia ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.

Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuvifanya vyama hivyo kuwa vyenye uwezo wa kujitegemea.

Katika hatua nyingine amesema serikali imeanzisha benki ya ushirika iweze kutoa huduma bora kwa vyama vya ushirika.