CCM yaahidi kuendeleza jitihada kukuza zao la korosho

Mtwara. Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendeleza mapinduzi katika sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika ruzuku ya pembejeo ili kuongeza uzalishaji, hasa wa korosho na mazao mengine kote nchini.

Akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 26, 2025 mkoani Mtwara, Samia amesema katika kipindi cha miaka minne pekee, Serikali imetumia Sh726 bilioni kugharamia pembejeo kwa wakulima nchini, wastani wa Sh152 bilioni kwa mwaka.

“Serikali yenu imeamua kuwekeza katika ruzuku kwa sababu tumedhamiria kukuza kilimo na kuongeza uzalishaji. Matokeo yake yameonekana wazi uzalishaji wa korosho umepanda kwa kiwango kikubwa. Kama isingekuwa mpango huu, leo tungekuwa tunashuhudia kuporomoka kwa uzalishaji,” amesema.


Mgombea huyo amebainisha kuwa jitihada hizo zimeifanya Tanzania kuwa namba mbili Afrika katika uzalishaji wa korosho, jambo ambalo amesema ni fahari kubwa, lakini pia changamoto kwa Serikali na wadau kuhakikisha jitihada zaidi zinafanyika ili kuongeza thamani ya zao hilo.

“Huu ni ushahidi kuwa tukiwekeza ipasavyo, tunaweza kushinda changamoto zote. Tunataka kuhakikisha wakulima wa Mtwara na maeneo mengine wanapata tija kubwa kupitia kilimo hiki. Kila korosho inayozalishwa itakuwa na soko la uhakika na bei nzuri,” ameongeza.


Amesema endapo atapata ridhaa ya kuongoza miaka mitano mingine, Serikali yake itaongoza juhudi za kutafuta masoko ya uhakika kwa mazao ya biashara, si korosho pekee bali pia mbaazi, ufuta na mazao mengine yanayolimwa kwa wingi nchini.

Katika mkakati wa kuongeza thamani ya mazao, mgombea huyo alibainisha kuwa Serikali itahakikisha inawavutia wawekezaji zaidi ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata korosho katika kongani iliyopo Kijiji cha Maranja mkoani Mtwara.

“Hatutaki kuona korosho zetu zikiuzwa ghafi na faida kubwa ikaenda nje ya nchi. Tunataka mnyororo mzima wa thamani ukae hapa kwetu kuanzia uzalishaji, uchakataji, hadi usafirishaji. Hii italeta ajira, kipato kwa wakulima na mapato kwa Serikali,” amesema.

Pamoja na hilo, amesema Serikali yake itaimarisha vyama vya ushirika ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikikabiliwa na changamoto za ubadhirifu wa fedha na ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.


“Tunataka vyama hivi vijengwe kuwa taasisi imara na za kuaminika, zinazoweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye kilimo chetu. Tukipata ridhaa ya wananchi, tutahakikisha vyama vya ushirika vinakuwa nguzo ya ustawi wa wakulima na sio chanzo cha kero,” amesema.

Samia amezungumzia pia Bandari ya Mtwara kwa kuruhusu korosho kusafirishwa kwa njia hiyo kwa kile alichoeleza ni hatua ambayo imepokewa vyema na watu wa mkoa huo.

“Mbali na korosho bandari hii ndiyo inasafirisha makaa ya mawe na ndiyo bandari pekee inayopokea pembejeo za kilimo katika ukanda wa kusini,” amesema.


Ameahidi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali yake itaanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati ya viwango vya kisasa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay mpaka Liganga na Mchuchuma.

“Imani yetu ni kwamba mradi huu si tu utafungua mkoa wa Mtwara bali ukanda wote wa kusini,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi baada ya mkutano huo, mkulima wa korosho kutoka Tandahimba, Juma Ali amesema ruzuku ya pembejeo imekuwa msaada mkubwa kwao kwani imesaidia kupunguza gharama za uzalishaji.


“Miaka ya nyuma tulikuwa tunahangaika kununua pembejeo kwa bei kubwa. Sasa tunapopewa bure, tija imeongezeka na hata kipato cha familia kinaboreshwa. Tunachoomba ni kuhakikisha ruzuku hii inaendelea,” amesema.

Kwa upande wake, Zainabu Athumani, mkulima kutoka Newala, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni ucheleweshaji wa malipo baada ya kuuza mazao yao kupitia vyama vya ushirika.

“Wakati mwingine tunakaa miezi kadhaa bila kulipwa. Hii inatuumiza kwa sababu tunahitaji fedha za kulipia ada, chakula na huduma nyingine. Tunafurahi kusikia kuwa Serikali imeahidi kulisimamia hili kwa ukaribu zaidi,” amesema Zainab.

Kwa upande wake Fatuma Rashid, mkazi wa Mtwara-Mikindani, amesema kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata korosho ndani ya mkoa huo kutakuwa suluhisho la ajira kwa vijana wengi.

“Kila msimu vijana wengi wanatafuta kazi za vibarua kwenye mashamba. Viwanda vikijengwa hapa, tutapata ajira za kudumu na kipato kitakachoboresha maisha yetu,” amesema Fatuma.