Dar es Salaam. Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Iringa, ACP Abdallah Misanya ameieleza mahakama kuwa barua ya nyongeza ya msamaha kwa wafungwa iliyowahusu raia watatu wa China waliokuwa wakitumikia kifungo katika Gereza la Ukonga, iliwasilishwa baada ya muda wa msamaha kupita.
Misanya, ambaye alishawahi kuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga kipindi cha Julai 2023 hadi Septemba 2023, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Septemba 26, 2025 wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili.
Mkama na wenzake, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa Gereza la Ukonga na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 25517/2024.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu raia wa China, wenye namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.
Inadaiwa kuwa Machi 18, 2016 wafungwa watatu wenye asili ya China, ambao ni mfungwa namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliohukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika gereza la Ukonga.
Wafungwa hao walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na wote walikuwa hawajuani.
Hata hivyo, Desemba 21, 2022, Mkama kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa gereza hilo na Nyabuya ambaye alikuwa ofisa Tehama wa gereza hilo kwa kipindi hicho, walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari ‘’Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.
Nyaraka hiyo ambayo ni barua ya Desemba 21, 2022, iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala akishirikiana na Eric Davies, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, shahidi huyo alidai kwa kawaida msamaha wa Rais huanza Novemba hadi Desemba 9, ambapo barua ya msamaha ikija na majina huifanyia kazi.
Alidai barua ya nyongeza ya msamaha wa Rais iliyowahusu wafungwa hao ilipita muda wa msamaha, kwani ilikuwa ya Desemba 27.
Misanya alidai , barua ya msamaha wa Rais hutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na inapelekwa kwa Kamishna Jenerali wa Magereza na kisha barua hiyo hushushwa kwa mkuu wa gereza wa Mkoa na mwisho hupelekwa kwa mkuu wa gereza husika.
Alidai, barua ya nyongeza ya msamaha inayohusu wafungwa hao, ilitoka moja kwa moja kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwenda kwa Mkuu wa gereza.
“Kimsingi si utaratibu sahihi barua itoke kwa Waziri kwenda kwa mkuu wa gereza na haikupaswa kusainiwa na Katibu Mkuu bali husainiwa na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani,” alidai shahidi
Misanya ambaye Julai 2023 hadi Septemba 2023 alipokea ukuu wa Gereza la Ukonga kutoka kwa Mkama alidai, alipopokea ukuu huo wa gereza hilo, alikuta mfungwa Song Lei, 205/2019 Xiu Fu Jie walishahamishwa gereza hilo.
Alidai mmoja alipelekwa gereza la Maweni Tanga na mwingine Gereza la Isanga, Dodoma.
Alidai, aliambiwa na watu wa utawala kwamba, wafungwa hao walihamishwa kutokana na kuzidi kwa malalamiko waliyokuwa wakiyatoa ya kutotolewa gerezani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 3, 2025 itakapoendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka.