Mbegu tano za parachichi zathibitishwa, wakulima mguu sawa kuanza kilimo

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kulipa kipaumbele zao la parachichi kutokana na mchango wake katika lishe, baada ya kusajili mbegu tano mpya ya zao hilo.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Septemba 23, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Nyasebwa Chimagu amesema wamesajili aina tano za parachichi ambazo ni Hass, Pinkerton, Fuerte, X-ikulu na Booth 7.

Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wakulima kupata miche yenye ubora uliothibitishwa na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Usajili huu wa aina za miche unalenga kumhakikishia mkulima anapata miche iliyo bora, jambo litakaloongeza kipato na tija katika sekta ya kilimo,” alisema Chimagu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Sura ya 308 na Kanuni za Mbegu za mwaka 2007, mbegu na miche yote inayouzwa lazima iwe imethibitishwa ubora wake na kusajiliwa.

Chimagu ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na malengo ya Serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata miche bora ili kuongeza ushindani wa zao la parachichi katika soko la kimataifa.

TOSCI imewataka wazalishaji na wauzaji wote wa miche ya parachichi kusajili mashamba ya miti mama kwa ajili ya uzalishaji wa vikonyo, kusajili vitalu vya uzalishaji wa miche bora ya parachichi inayobebeshwa, na kusajili vitalu vya uzalishaji wa miche bora iliyobebeshwa.

Usajili huo unatakiwa kufanyika ndani ya siku 90 kuanzia tarehe ya tangazo. Baada ya muda huo kupita, TOSCI itachukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaobainika kukiuka utaratibu huo.

Hatua hii imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali kuhakikisha zao la parachichi linakuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na sekta binafsi, sambamba na kuongeza pato la taifa kupitia mauzo ya nje.

Hali ya mauzo ya parachichi

Kulingana na Hotuba ya bajeti  Wizara ya Kilimo 2024/2025 uzalishaji wa zao la parachichi zinazouzwa nje ya nchi, umeongezeka kutoka tani 17,711 mwaka 2021/22 hadi tani 26,826 mwaka 2022/23.

Ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa soko la ndani na nje ya nchi ambapo tangu mwaka 2020/21  Wizara ya Kilimo imebaini tani 15,432 za parachichi zenye thamani ya Sh102.1 bilioni ziliuzwa.

Tanzania ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa zao hilo Barani Afrika, huku soko kubwa la parachichi likiwa katika nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza, Uholanzi na nchi za China na India kwa upande wa Asia.

Hivyo, kuimarishwa kwa ubora wa uzalishaji wa zao hilo kunatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi kupitia ongezeko za mauzo ya mazao nje ya nchi.