Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema Serikali atakayoiunda itahakikisha shughuli zote zinazopaswa kufanywa na Wazanzibari, zinafanywa na wenyewe badala ya wageni.
Othman maarufu ‘OMO’ amesema hatua hiyo, itasaidia faida itakayopatikana kubakia katika mzunguko wa fedha Zanzibar, ili kupunguza ukali na ugumu wa maisha kwa Wazanzibari.
Othman amesema hayo leo Ijumaa Septemba 26,2025 akihubutia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika viwanja vya Stella Darajabovu, Jimbo la Welezo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mgombea huyo, leo ameendeleza kampeni zake baada ya jana Alhamis Septemba 25,2025 kusitisha jimbo la Bumbwini, kupisha msiba wa Abbas Mwinyi ambaye ni kaka wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Abbas alifariki usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi Lumumba alipokuwa akiendelea na matibabu na amezikwa leo Septemba 26, katika makaburi ya familia Mangapwani, Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akihutubia wananchi hao, Othman ameeleza, “Mfano pale uwanja wa ndege kulikuwa na kampuni ya wazawa ikitoa huduma ikijiri watu 400 wote walitoka Zanzibar. Kuna kampuni ya ndugu zetu Zanzibar, iliajiri watu 230, lakini sasa hivi zimeondolewa kwa wakati mmoja,” amedai Othman.
Na kuongeza kuwa, “leo nendeni uwanja wa ndege, kaulize walioajiriwa walikotoka. Hii ndio ilikuwa faida ya wazawa kushiriki katika uchumi, sasa sera yetu katika uwezeshaji, mkinipigia kura wajibu wangu wa kwanza ni Wananchi,” amesema.

Othman amesema endapo Wazanzibari Oktoba 29, 2025 wakimchagua Serikali atakayoiongoza, biashara yoyote itakayoweza kufanya na Mzanzibari mwenye uwezo, basi Serikali itamwezesha aifanye.
“Kwenye hili ACT Wazalendo hatutakuwa na muhali, wala sitoona aibu kwa sababu wajibu wangu wa mwanzo ni kuwatoa kwenye umasikini bandia mlionao huu. Hii ndio kazi ya Serikali mtakayonikabidhi,”
“Wazanzibari mnaweza kufanya kila kazi, aliyekuwa fundi selemala kazi yetu kumtafutia maarifa na mtaji ili kuzalisha kiwango cha kuuza bidhaa yake popote,” ameeleza Othman.
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, amefafanua kuwa uwezeshaji hautaji fedha nyingi, bali Mawazo na Serikali inayowajali wananchi wa Zanzibar.
“Leo ukitaka kijola lazima uvuke maji uende Dar es Salaam…kweli? au ukitaka chombo unavuka maji,” ameeleza.
Othman amewaambia wananchi wa Zanzibar kuwa uchaguzi wa mwaka huu, si wa kumtafutia Othamn kura au ACT Wazalendo bali kuinusuru na kuirejesha heshima ya Zanzibar.
“Nazungumza kwenye jimbo la wananchi kwelikweli, shida na dhiki za maisha, Welezo, dhahama zikitokea zipo Welezo. Hili ni jimbo la wananchi, tunazijua shida zenu, hatuhitaji kufundishwa,” amesema Othman.
Meneja wa kampeni wa ACT Wazalendo,” Ismail Jussa amesema ,“tunaposema 2025 ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar, ni pamoja na ahadi zisizotekelezeka zilizotolewa na viongozi walioko madarakani,” ameeleza Jussa.
Awali Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman amesema baada ya jana Alhamisi kuahirisha mkutano wa Bumbwini kutokana na msiba, sasa utafanyika Jumapili Septemba 28.