Dar es Salaam. Siku moja tulishuhudia mtanange wa soka wa kushangaza sana. Lilikuwa “Ndondo Cup” enzi hizo likipigwa mchangani. Wengine walicheza peku, na timu iliyopungukiwa na jezi ilicheza matumbo wazi. Siku hiyo timu ya kitaani iliyokuwa bingwa mtetezi ilicheza fainali dhidi ya mahasimu wao wakubwa.
Walipokutana hawa ilikuwa kama Simba na Yanga, kitaa kizima kilinuka. Lakini siku hiyo timu ya mtaani kwetu ilikuwa dhaifu sana, maana mastaa wengi walinyakuliwa kwenye ligi ya Taifa.
Alichoweza kufanya kocha wetu ni kumuibua na kumnoa dogo mmoja. Huyu dogo alikuwa ndiye tumaini la pekee kwa timu, aliweza kupiga mabao kwa kadiri alivyojisikia. Hata kama wapinzani wangeweza kufunga mabao sita, dogo alisawazisha na kuwapiga la kuongoza.
Huyu dogo alikuwa mdomoni mwa kila mtu, na kwa bahati nzuri kila alipoitwa kwenda kucheza ligi alidharau. Alisema “bongo hakuna hela ya kunilipa”. Lakini mgema akisifiwa mambo yanaharibika. Sasa dogo akawa ni lazima abembelezwe kwa pesa kabla hajaingia uwanjani.
Kumbe alishaanza kunusa poda mdogomdogo hadi akaingia chama la waraibu. Mwanzoni wote tulidhani anavuta bangi tu, kumbe hali ilishakuwa mbaya. Kocha akaanza kumkataa, na yeye mwenyewe akajikataa. Alikuja uwanjani kuvuta bangi na wahuni, na si kucheza kandanda.
Sasa siku hiyo sabu iliyochukua namba yake ilikuwa majeruhi. Bahati mbaya hakukuwa na mchezaji mwingine aliyefiti kwenye namba ile. Wakati mahangaiko yakiendelea mpira ukaanzishwa. Dakika tano za mwanzoni tulishakoswa mabao matatu ya wazi. Mdau mmoja baada ya kuona jahazi likididimia, alikwenda kuteta na kocha.
Akatoa pochi na kumkabidhi dogo hela ya “dawa”. Dogo alitoka mbio kama kaiba, alikimbilia nyuma ya ukuta wa shule na fasta akarudi mchangamfu. Akaomba jezi kwa kocha, na kocha hakuwa na jinsi bali kufanya mabadiliko. Ile kuingia tu, dogo akautafuta na kuunasa mpira.
Alipiga chenga kila mtu pamoja na wachezaji wa timu yake. Cha kushangaza alielekea golini kwao. Akampiga chenga kipa wake na kumtungua bao. Mashabiki walichanganyikiwa lakini yeye aliwatuliza kwa mikono akiwaashiria wasubiri. Akaunasa tena na kuelekea golini kwa adui akasawazisha na kupiga bao mbili za ushindi.
Nimeikumbuka hiyo baada ya kumsikia mgombea urais wa Zanzibar kupitia upinzani akiipiga bao kambi yake mwenyewe. Akizungumza baada ya kukabidhiwa gari kwa ajili ya kampeni, mgombea huyo alimtakia ushindi mwema mgombea wa CCM kama vile amesahau yeye ni mgombea pia (tena wa kutoka upinzani). Nisiwe mnafiki, sikuweza kusikia maneno yake ya mwisho kwani nilijikuta nikicheka muda wote.
Kikubwa ni kwamba jamaa anafanya vituko hivyo akitambua hali ilivyokuwa tete kwenye kambi yake. Anafanya kama kumgongelea msumari wa utosi mgonjwa asiyejiweza kitandani. Maana imefikia mahala nikajisemea “nilijua kuwa wapinzani wamechoka, lakini sikujua kuwa ni kwa kiasi hiki!” Naamini hata kama mfadhili ataamua kuwasaidia, atajiuliza mara mbili: “Hawa wakipewa magari wanachanganyikiwa, je wakipewa nchi?”
Pengine mgombea huyu anafanana na yule dogo straika wetu aliyejipiga bao moja, na kutuomba tusubiri apige mawili ya ushindi. Nasema wanafanana kwa sababu alinikumbusha dogo kwa mara ingine alipokuwa akikana kuvuta mjani. Sijui mtangazaji alihisi nini, au kuna watu walimsanua kuwa mgombea huyo naye anaukoka mjani. Watu wanasema ukipiga mistari unaona kama unatembea hewani vile… Aaakh! Tuyaache hayo, maana wengine mnaniangalia kwa udadisi.
Kuchoka kwa wapinzani kulianzia pale chama kikuu cha upinzani kilipojiondoa kwenye kinyang’anyiro. Chadema hawakukubaliana na sheria za uchaguzi kwa madai kuwa zinaubeba upande wa watawala, na mgombea wake wa Urais akashtakiwa kwa kosa la uhaini. Lakini nyundo ingine ikatua kichwani pale mgombea urais kupitia ACT Wazalendo alipopigwa breki akiwa hewani. Angalau huyu ndiye angebeba matumaini ya wapinzani baada ya kukosekana Tundu Lissu.
Nyundo ya tatu ambayo wengi hawaioni, ni ile ya wagombea urais wa kambi ya upinzani kukariri maneno ya mgombea wa CCM. Chama tawala kimesema kuwa kinanuia kuboresha maisha ya Mtanzania, kitatoa elimu na afya bure. Kila chama cha upinzani kimeyarudia maneno hayo, tena bila kujali kuwa huo ni kama wimbo unaorudiwa kwenye kila awamu. Hawajiongezi kuwa wananchi wameshausikiliza kwa muda mrefu, sasa labda uwapigie “rimix” ndo utawakonga.
Tazama mistari hii: Wimbo wa chama tawala unasema “Tutaleta katiba mpya katika miezi kumi na mbili baada ya kuingia mjengoni”. Wa upinzani nao unaimbwa “Tutaleta katiba mpya katika miezi kumi baada ya kuingia mjengoni”. Hapa kama ingelikuwa ni wagonga singeli si wangepelekana Cosota? Au tutasema wote wamepandia mistari ya prodyuza kama alivyokuwa akifanya “Majani”; anagonga biti halafu anaigawa kwa wasanii tofauti.
Leo naona niishie hapa. Lakini nimewaandalia wasomaji wangu ukurasa wa facebook unaokwenda kwa jina la “Hekaya za Mlevi”. Soma makala za kitambo zilizoombwa na wengi, lakini like, share na subscribe usome kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025. Ni jambo la msingi msomaji wangu ujitokeze Oktoba 29 ili kutimiza haki yako ya msingi kupiga kura. Lakini chonde usije ukaingizwa mjini. Nasikia mgombea mmoja anakuja kuahidi ati mkimchagua mtaingia peponi!