Bado Watatu – 41 | Mwanaspoti

AFISA upelelezi akauliza kwenye simu:
“Natumaini naongea na mstaafu Hashim Malick?”
“Hapana. Unaongea na daktari mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza. Mzee Hashim Malick amepata ajali ya gari dakika chache zilizopita. Ameletwa hapa akiwa hajitambui pamoja na dereva wake.”
Maelezo hayo yalimshitua afisa upelelezi.
“Unasema amepata ajali ya gari?” akauliza.
“Ndiyo. Gari lake limegongana na lori la mafuta, kilometa tatu kabla ya kuingia Muheza, akitokea Hale.”
“Ajali imetokea muda gani?”
“Dakika chache zilizopita tu. Ameletwa hospitalini na sasa tunajaribu kupokea simu zake ili kuwasiliana na ndugu zake.”
“Ndani ya gari lake kulikuwa na watu wangapi?”
“Alikuwa ni yeye na dereva wake na wote wameumizwa.”
“Umesema Hashim Malick hajitambui?”
“Hajitambui. Madaktari ndio wanajaribu kuokoa uhai wake.”
“Hali ikoje kwa dereva wake?”
“Dereva wake anaweza kuzungumza, ingawa siwezi kusema kwamba ana afadhali sana.”
“Mimi ni afisa upelelezi wa mkoa. Nilikuwa namuhitaji Hashim, itabidi nifike hapo haraka kumuona.”
“Sawa.”
Afisa upelelezi alikata simu akaniambia:
“Hashim Malick amepata ajali na yuko mahututi, itabidi twende Hospitali ya Muheza.”
“Sawa, twende.”
Tukatoka tena. Safari hii niliendesha mimi. Tulipofika Muheza tulikwenda katika Hospitali ya Wilaya na kujitambulisha kwa mganga mkuu.
“Nasikitika kuwambia kwamba majeruhi mmoja ameshatutoka,” mganga mkuu akatuambia.
Sote tukashituka.
“Ni yupi?” Afisa upelelezi akauliza.
“Bwana Hashim ametutoka. Kumbe ni afisa mstaafu wa Gereza la Maweni.”
“Nani alikwambia?”
“Dereva wake. Ametuambia kwamba yeye pia alikuwa askari wa magereza na alikuwa dereva wake tangu wakiwa katika jeshi hilo.”
“Hebu twende tukamuone.”
Mganga mkuu akatupeleka katika chumba cha maiti na kutuonesha mwili wa Hashim Malick uliokuwa umetapaa damu.
Tulipotoka chumba cha maiti, akatupeleka katika chumba alichokuwa amelazwa dereva wake.
Alikuwa amefungwa bendeji sehemu mbalimbali za mwili wake na alikuwa akiwekewa damu. Alionekana kuwa mahututi.
Hata hivyo alipotuona aligeuza macho na kututazama.
“Unajisikiaje?” Afisa upelelezi akamuuliza.
“Ninakufa. Mimi ni askari mstaafu wa jeshi la magereza. Nilikuwa dereva wa mkuu wa gereza na hata nilipostaafu, mkuu huyo aliniajiri niwe dereva wake mpaka hii leo tulipopata ajali pamoja.”
“Nimekuelewa. Kwa nini unasema unakufa?”
“Sitapona. Nimeumia vibaya sana. Naomba kila niliyemkosea anisamehe.”
“Hujatukosea kitu. Mimi ni afisa upelelezi wa mkoa huu. Nilikuwa namuhitaji bwana Hashim lakini kwa bahati mbaya ndiyo ametutoka.”
“Kumbe bwana Hashim amekufa? Mimi sijui kama amenitangulia.”
Nilihisi kwamba afisa upelelezi aligundua kosa lake la kumwambia mtu huyo kuwa mwenzake ameshakufa. Akamtuliza.
“Usiwe na wasiwasi. Utapona tu.”
“Sidhani. Mimi naona kama ninasubiri wakati tu.”
“Ulipokuwa katika jeshi la magereza ukimuendesha mkuu wa gereza hilo, kitu gani kilitokea?”
“Vitu vingi vilitokea. Siwezi kujua unakusudia kitu gani.”
“Unajua tulikuwa tunamtaka Hashim kwa ajili ya kumhoji kuhusu watu wanne waliohukumiwa kunyongwa lakini walikuja kuonekana tena mitaani na katika makaburi yao kulikuwa na maiti wengine.”
“Umenikumbusha kitu muhimu. Nilikuwa najaribu kuyakumbuka makosa niliyofanya katika maisha yangu na watu niliowakosea ili niombe msamaha kwa Mungu kabla ya mauti yangu. Sasa umenikumbusha kitu muhimu.”
Mimi na afisa wangu tukapata shauku ya kumsikiliza askari huyo mstaafu wa magereza aliyekuwa dereva wa mkuu wa Gereza la Maweni.
Kwa vile alinyamaza kidogo, afisa upelelezi akamuuliza:
“Ni kitu gani muhimu ulichokumbuka?”
“Bila shaka wafungwa uliowataja ni wa familia ya Unyeke?”
“Bila shaka. Wewe utakuwa unajua.”
“Kuficha ukweli ni dhambi. Mimi ninajua kila kitu kilichotokea. Nilificha ukweli wakati huo, lakini kwa saa yangu hii ya mauti siwezi kuficha tena. Hashim Malick mwenyewe ameshanitangulia mbele ya haki.”
“Sasa tueleze huo ukweli ni upi,” afisa upelelezi akamwambia.
“Mke mdogo wa Hashim Malick alikuwa ni Miriam Unyeke. Alikuwa mtoto wa mwisho wa mzee Unyeke. Wale jamaa wanne waliohukumiwa kunyongwa walikuwa ni mashemeji wa Hashim Malick. Miriam alimuomba Hashim awanusuru ndugu zake kwa vyovyote atakavyoweza.”
Askari huyo mstaafu akaendelea kutueleza:
“Mimi nimeyajua hayo si kwa sababu nilikuwa dereva wa Hashim bali nilikuwa mpambe wake. Hata wakati anamtongoza Miriam mimi nilichangia sehemu kubwa hadi wakawa wamoja.”
“Ndiyo, endelea,” afisa upelelezi akamwambia.
“Baada ya kaka zake Miriam kuhukumiwa kunyongwa, Miriam alipata pigo kubwa sana la kuwapoteza ndugu zake hao. Alikuwa hali, hanywi. Kila siku alikuwa anamlilia Hashim ajaribu awezavyo kuwanusuru ndugu zake. Baada ya kuwaza na kufikiri ndipo Hashim alipobuni mpango wa kuwatoa kwa hila. Kwa vile alikuwa bosi wangu na pia rafiki yangu, alinihusisha katika mpango huo.”
“Tueleze huo mpango ulivyokuwa?”
“Unajua Hashim alikuwa katili na alikuwa akijiamini katika mipango yake. Mwaka ule kulikuwa na wafungwa wanne waliohukumiwa kunyongwa ambao walitakiwa kuachiwa kwa msamaha wa rais. Kwa kawaida ile hati ya kuwaachia wafungwa inakuja moja kwa moja kwa mkuu wa gereza na inakuwa ni siri yake labda kama atatangaza yeye mwenyewe…”
Askari huyo mstaafu alinyamaza, akapepesa macho kama ambaye alikuwa anajaribu kuvuta kumbukumbu kisha akaendelea:
“Ile hati ya kuwasamehe wafungwa hao ilikuja sambamba na hati ya kuwanyonga kina Unyeke kutoka kwa rais. Alichofanya Hashim, aliwanyonga wale watu wanne waliosamehewa akawaachia kina Unyeke…”
Askari huyo alinyamaza tena akiendelea kupepesa macho kabla ya kuendelea:
“Ili kuficha dhambi yake Hashim aliandika kwamba aliwanyonga kina Unyeke kumbe sivyo. Hili jambo lilifanyika kwa usiri mkubwa na halikufahamika. Hata aliyewanyonga wale wafungwa hakujua kuwa aliwanyonga watu wasiotakiwa kunyongwa.”
“Ndiyo,” afisa upelelezi akamuitikia kwa namna ya kumhimiza aendelee kueleza.
“Kwa bahati njema mwaka ule ule Hashim akastaafu. Mwaka uliofuata nikastaafu mimi. Kwa vile tulikuwa bado marafiki, nilipostaafu akaniajiri kazi ya udereva. Hadi hii leo tumepata ajali, mimi ndiye nilikuwa dereva wake.”
Afisa upelelezi akanitazama. Na mimi nikamtazama kisha nikatingisha kichwa kuonyesha kuelewa kilichotokea.
“Kumbe ilikuwa hivyo?” Afisa upelelezi akamuuliza askari mstaafu aliyekuwa akitupa hadithi hiyo.
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Na sikujua kama ingegundulika. Hashim aliwaambia wafungwa wake aliowaachia wabadili majina na huko uraiani wasijichanganye na watu wanaowajua.”
Afisa upelelezi akanitazama tena kabla ya kuurudisha uso wake kwa askari huyo mstaafu.
“Huyo Miriam ambaye ni bibi yake Hashim yuko wapi?”
“Miriam alishakufa. Alifia Muhimbili baada ya kupata kansa ya ini mwishoni mwa mwaka jana.”
“Wakati huo ndugu zake walikuwa wameshaachiwa?”
“Ndiyo, walikuwa wameshaachiwa.”
“Hili jambo linafahamika wakati Hashim ameshakufa. Kwa upande wake kufa si bahati mbaya. Huko aliko anashukuru kwamba jambo hilo limefahamika wakati yeye ameshakufa,” afisa upelelezi alisema akiwa amekasirika.
“Na mimi ndiyo nimeweza kusema kwa kujua kuwa Hashim amekufa na mimi nitakufa.”
“Wewe pia ulifanya kosa kwa kuficha siri ya hatia kama hiyo.”
“Ndiyo maana ninaungama kwa Mungu na huwezi kuungama hadi uyataje mabaya yako.”
“Lakini afande, kuna kosa jingine la kuwanyonga watu waliokwishasamehewa. Lingekuwa ni kosa la mauaji,” nikamwambia afisa upelelezi.
“Ninajua. Yote ni makosa. Huyu bwana amefanya mambo makubwa sana.”
Wakati huo askari huyo mstaafu alikuwa amenyamaza kimya.
Tukaona hali yake ikianza kubadilika. Alianza kupumua kwa nguvu kisha mwili wake ukaanza kulegea.
“Hujisikii vizuri?” Afisa upelelezi akamuuliza.
Askari huyo hakujibu chochote. Alikuwa kama hayuko na sisi. Alikuwa akiendelea kupumua.
Wakati tumo kwenye gari tukirudi jijini Tanga, afisa upelelezi aliniambia:
“Pamoja na kwamba Hashim ameshakufa na hawezi kushitakiwa, lakini tumejua kilichotokea.”
“Tumejua kilichotokea lakini bado kuna utata mwingine.”
“Utata upi?”
“Ni nani aliyewanyonga kina Unyeke?”
“Tunakwenda hatua kwa hatua. Tumemaliza hatua moja, sasa tunakwenda kwenye hatua nyingine ya kumjua huyo muuaji.”
“Uchunguzi wangu hadi sasa hivi umeonesha muuaji ni Thomas. Lakini Thomas huyo naye alishauawa na kina Unyeke.”
“Unataka uniambie kuwa alirudi duniani kulipa kisasi kwa kina Unyeke?”
Afisa upelelezi aliponiuliza hivyo, tulicheka sote.
“Ni kama hivyo, lakini huyu mtu inaonekana yupo, kwa sababu alama ya dole anayoiweka katika karatasi anazoziacha kwa marehemu ni yake.”
“Kweli, huo ni utata. Unatakiwa uushughulikie kuanzia sasa.”