Tanzania Prisons, KMC leo patachimbika

BAADA ya kila moja kutoka kupoteza mechi zilizopita za Ligi Kuu Bara, Tanzania Prisons na KMC zinashuka uwanjani kuvaana leo, huku makocha  wakitambiana ili kuepuka aibu mwisho wa msimu.

Prisons imepoteza mechi mbili zilizopita mbele ya Coastal Union na Namungo ugenini wakati KMC iliyoanza na ushindi dhidi ya Dodoma Jiji ilipasuka mechi iliyopita mbele ya Singida Bl;ack Stars na leo zitajiuliza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Kocha Mkuu wa Prisons, Zedekia Otieno alisema jana kuwa leo anaanza rasmi kazi kwa kuifumua KMC akiwataka nyota wake kujituma.

Otieno alisema mastraika wanamuangusha akieleza kwa sasa anaendelea kutengeneza timu baada ya kikosi kuondokewa na wachezaji wanane.

Kocha huyo anayefundisha kwa mara ya kwanza Tanzania aliliambia Mwanaspoti kwamba katika mechi zilizopita walizopoteza ugenini mastraika hawakuonyesha makali aliyotarajia licha ya kutengeneza nafasi nyingi.

Alisema kwa sasa anatengeneza muunganiko wa timu akiamini kuanzia mchezo huo Prisons haitashikika kwa kutembeza vipigo. “Tumepoteza mechi zote za ugenini, lakini timu haijacheza vibaya badala yake ni makosa madogo kwenye eneo la ushambuliaji kutotumia nafasi walizopata. Nachotaka wajitume,” alisema kocha huyo.

Mkenya huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa nchini humo ikiwamo Gor Mahia msimu uliopita na timu ya Taifa ‘Harambee Stars’ alisema hawatadharau mechi kwa kuwa wapinzani wao siyo wa kubezwa.

Akizungumzia mechi hiyo, nyota wa KMC, Samson Mwakyusa alisema wanaingia uwanjani kwa umakini ili kuhakikisha hawafanyi makosa kama ilivyokuwa dhidi ya Singida Black Stars.

Alisema benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Marcio Maximo liliyabaini makosa na kuwapa mbinu kuwakabili Prisons ili kupata pointi tatu. “Kocha ametupa mbinu na sisi wachezaji hatutarajii kurudia makosa. Tunajua Prisons wapo nyumbani na hawajashinda mechi yoyote. Presha itakuwa kubwa ila tunataka pointi tatu,”  alisema nyota huyo aliyewahi kupita Prisons.

Kocha wa timu hiyo, Maximo alisema pamoja na kutafuta matokeo, lakini hesabu zake ni kutengeneza timu ya miaka sita hadi 10 ijayo kuwa bora ndani na nje akisifia kikosi kilichopo.

“Miundombinu bora ipo. Uongozi una mipango mikubwa na mirefu. Kwa maana hiyo nataka nitengeneze timu ya miaka sita au 10 mbele yenye mafanikio ndani na nje,” alisema.

“Ukiangalia Ligi Kuu ya sasa Tanzania imebadilika, binafsi naiona kama ya kwanza Afrika kwa kuwa inavutia na ushindani ni mkubwa.